Nov 14, 2021 08:16 UTC
  • Askari 2 wa Uganda wahukumiwa kifo kwa mauaji ya raia Somalia

Askari wawili wa Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) wanaohudumu kwenye Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) wamehukumiwa kifo, kutokana na mauaji ya raia katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Katika hukumu yake mjini Mogadishu, Mahakama Kuu ya Kijeshi aidha imewahukumu wanajeshi wengine watatu wa UPDF kifungo cha miaka 39 jela kwa kuhusika na mauaji hayo ya raia wa Kisomali mnamo Agosti 10 mwaka huu.

Mauaji hayo ya raia saba wasio na hatia katika eneo la Golweyn lililoko eneo la Lower Shabelle kusini mwa Somalia, yapata kilomita 110 kusini mwa mji mkuu Mogadishu yaliibua hasira miongoni mwa wananchi wa Somalia, ambapo mamia miongoni mwao walifanya maandamano ya kulaani ukatili huo. 

Timu ya AMISOM iliyochunguza tukio la mauaji hayo ilizipa mamlaka za Uganda jukumu la kuwafungulia mashtaka askari waliohusika na mauaji ya raia saba wa Somalia.

Askari wa Uganda ambao ni sehemu ya kikosi cha AMISOM nchini Somalia

Taarifa iliyotolewa na timu hiyo mwezi uliopita ilisema: "Kwa masikitiko, watu saba waliouliwa walikuwa raia; na utendaji wa askari waliohusika ulikiuka kanuni za utendaji za AMISOM."

AMISOM inaundwa na askari 22,000 kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone, aghalabu ya wanajeshi hao wakiwa ni Waganda.

Tags