Nov 15, 2021 11:48 UTC
  • Nigeria yashambulia asasi ya Marekani kwa kuipaka matope

Serikali ya Nigeria imeijia juu asasi moja isiyo ya kiserikali ya Marekani iliyodai kuwa, utawala wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi unaunga mkono ugaidi.

Katika taarifa, Waziri wa Habari na Utamaduni wa Nigeria, Lai Mohammed ametaja tuhuma hizo zilizotolewa na shirika la Global Advocates for Terrorism Eradication (GATE) kama madai ya kuchukiza, na yaliyotolewa na wenye lengo la kudhoofisha vita vinavyoendelea dhidi ya magenge ya kigaidi na wabeba silaha katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Waziri Mohammed amebainisha kuwa, shirika hilo la Kimarekani linalodai kufanya kampeni za kukabiliana na ugaidi duniani linapaswa kupuuzwa kwa kuwa limechanganyikiwa na halina maana.

Amesema, "shirika hilo la GATE halina maana wala umuhimu wowote. Inawezekanaje shirika ambalo ni la uhakika kuituhumu serikali inayopambana na jinamizi la ugaidi na ujambazi, kuwa inafadhili ugaidi?"

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Waziri wa Habari na Utamaduni wa Nigeria ameongeza kuwa, serikali ya Abuja itaendelea kupambana na ugaidi wa ndani ya nchi na wenye mfungamano na magenge ya kigaidi ya dunia.

Shirika la GATE hivi karibuni liliitaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuwaweka baadhi ya maafisa wa serikali ya Nigeria katika orodha ya eti 'waungaji mkono wa ugaidi' likidai kuwa, dalili zote zinaashiria kuwa, kinachofanyika nchini Nigeria hivi sasa ni ugaidi unaofadhiliwa na serikali.

 

 

Tags