Nov 16, 2021 16:51 UTC
  • Algeria na Afrika Kusini zapinga tena Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika AU

Algeria na Afrika Kusini zimetangaza tena msimamo wao wa kupinga utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika, AU.

Sisitizo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Ramtane Lamamra na Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini Naledi Pandor, katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo yao ya pande mbili.

Mbali na kutilia mkazo msimamo wao kupinga utawala wa Kizayuni kukubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji wa AU, mawaziri hao wa Algeria na Afrika Kusini wamesema, Algiers na Pretoria zinaheshimu suala la umoja katika AU kulingana na misingi na malengo yaliyoainishwa kwenye hati ya kuasisiwa taasisi hiyo, lakini zinatahadharisha juu ya hatari yoyote inayotishia mshikamano wa Umoja wa Afrika.

Katika kikao cha mwisho cha AU, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo wa Afrika.

Uamuzi huo ambao ulichukuliwa na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki umekosolewa vikali na nchi nyingi wanachama wa AU zikiwemo za Kiarabu za eneo Afrika Kaskazini.

Nchi hizo zinaamini kuwa, kukubaliwa Israel kuwa mwanachama katika Umoja wa Afrika ni sawa na kuyapa mgongo na kuyadharau malengo matukufu ya taifa la Palestina.

Algeria, ikishirikiana na nchi zingine 13 wanachama wa Umoja wa Afrika, imetaka kufutwa uwanachama huo wa utawala wa Kizayuni katika AU na kulindwa hadhi na thamani ya asasi hiyo kuu ya bara la Afrika.../

Tags