Nov 19, 2021 07:39 UTC
  • Algeria yafunga ofisi zake sita za kibalozi nchini Ufaransa

Katika kile kinachoonekana ni kuendelea kuvurugika uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ufaransa na Algeria, serikali ya Algiers imetangaza habari ya kufunga balozi zake ndogo zipatazo sita katika nchi hiyo ya Ulaya.

Rais wa Algeria, Abdulmajid Tabboune ametangaza kuwa, nchi hiyo imesitisha shughuli za balozi zake ndogo nchini Ufaransa katika miji ya Nice, Toulouse, Crete, Pontoise, Montpellier na Bobini.

Hatua hiyo ya Algiers imechukuliwa huku uhusiano wa pande hizo mbili ukiendelea kuyumbayumba baada ya matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhusu historia ya Algeria yaliyotambuliwa na Waalgeria kuwa ni dharau na kudhalilishwa nchi yao. 

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya rais huyo kukataa mwaliko wa Ufaransa wa kushiriki mkutano wa Paris ulioitishwa kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini Libya.

Kushtadi mvutano baina ya Ufaransa na koloni lake la zamani

Mwezi uliopita gazeti la Le Monde la Ufaransa lilimnukuu Emmanuel Macron akimshambulia kwa maneno ya jeuri Rais wa Algeria na kusema kuwa historia ya Algeria inapaswa kuandikwa upya. Macron alidai kuwa, hakukuwa na taifa liitwalo Algeria kabla ya kuvamiwa ardhi za nchi hiyo na wakoloni wa Ufaransa. Waalgeria wamekasirishwa mno na maneno hayo ya kifidhuli ya Rais wa Ufaransa.

Algeria ilimwita nyumbani balozi wake wa Ufaransa kwa ajili ya mashauriano ikilalamikia matamshi hayo yaliyotolewa na Rais wa Emmanuel Macron dhidi ya nchi hiyo, ambayo Algiers iliyataja kama ya upotoshaji na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Tags