Nov 19, 2021 11:55 UTC
  • Washukiwa watano wa miripuko ya kigaidi Uganda wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi

Polisi ya Uganda imesema, imewaua kwa kuwapiga risasi washukiwa watano na kuwatia nguvuni watu 21 kufuatia miripuko pacha ya mashambulio ya mabomu ya siku ya Jumanne iliyopita, ambayo iliua watu wasiopungua watano na kujeruhi makumi ya wengine katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala.

Msemaji wa polisi Fred Enanga amewaeleza waandishi wa habari kuwa, askari wa kikosi cha kupambana na ugaidi waliwaua kwa kuwapiga risasi washukiwa wanne wa ugaidi huko Ntoroko, walipokuwa wakijaribu kuvuka mpaka kurejea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa Enanga, mtu wa tano aliyejulikana kama Sheikh Abas Muhamed Kirevu, aliuliwa karibu na mji mkuu Kampala alipokuwa anajaribu kutoroka asikamatwe; na akaongeza kuwa, Kirevu alikuwa kiongozi wa Kiislamu ndani ya Uganda mwenye jukumu la kufufua tena vikundi vidogovidogo vya kigaidi mjini humo.

Aidha amesema, polisi imewakamata watuhumiwa 21, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kulisambaratisha kundi linalobeba silaha liitwalo Vikosi vya Muungano wa Kidemokrasia, Allied Democratic Forces (ADF), ambalo linaendesha harakati zake mashariki ya Kongo DR, na ambalo Marekani inalihusisha na genge la kigaidi lijiitalo Dola la Kiislamu la Iraq na Sham, DAESH (ISIS).

Wanamgambo wa ADF

Miripuko ya kigaidi ya siku ya Jumanne katika mji mkuu Kampala ilipishana kwa dakika chache, ambapo washambuliaji wawili wa kujitoa mhanga waliopanda pikipiki wakijifanya madereva wa bodaboda, walijiripua karibu na jengo la bunge, huku mshambuliaji wa tatu akilenga kuripua kitu cha upekuzi karibu na makao makuu ya polisi jijini humo.

Mashambulio hayo pacha ambayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua wanne na kuwajeruhi wengine zaidi ya 33, ni hujuma ya karibuni zaidi kuilenga nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Kundi la ADF lilitangaza kuhusika na shambulio la bomu lililotokea mwezi uliopita karibu na mkahawa maarufu wa Kawempe jijini Kampala.

Kwa muda mrefu, kundi hilo la kigaidi limekuwa likipinga utawala wa Rais Yoweri Museveni, kiongozi wa muda mrefu wa Uganda na muitifaki wa kiusalama wa Marekani, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kiafrika kutuma askari wa kulinda amani nchini Somalia ili kuihami serikali kuu ya nchi hiyo dhidi ya hujuma za kundi la kigaidi la Ash-Shabaab.../

Tags