Nov 22, 2021 12:28 UTC
  • Covid-19; Wasiochanja kutopewa huduma muhimu za serikali Kenya

Wananchi wa Kenya ambao hawajapiga dozi kamili ya chanjo ya Covid-19 watanyimwa hudumu muhimu zinazotolewa na taasisi za serikali ya nchi hiyo kuanzia mwezi ujao wa Disemba.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe amewaambia waandishi wa habari kuwa, serikali imeamua kuchukua maamuzi hayo magumu kwa lengo la kuwakinga Wakenya wote dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Amesema baadhi ya huduma ambazo Wakenya ambao hawajachanja watakosa kupewa ni pamoja na huduma za Mamlaka ya Mapato (KRA), elimu, uhamiaji, bandari, Mamlaka Taifa ya Usalama Barabarani (NTSA), hospitali na hata kuwazuru wafungwa magerezani.

Waziri Kagwe amesisitiza kuwa, serikali haitaruhusu Wakenya ambao wamechanja wahatarishe maishe yao kuwahudumia wale ambao wamekataa kupiga chanjo kwa makusudi.

Hii ni katika hali ambayo, kiwango cha maambukizi nchini humo kimepungua kwa kiasi kikubwa, ambapo hivi sasa asilimia  0.7. Jumla ya Wakenya 254,710 wameambukizwa virusi vya Corona kufikia sasa, huku idadi ya walioaga dunia kwa maradhi hayo ikipindukia 5,300.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe 

Mwezi uliopita, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliondoa marufuku ya kutembea usiku ambayo ilikuwa ikitekelezwa tangu mwaka jana 2020, baada ya maambukizi ya Corona kupungua nchini humo.

Watu karibu milioni nne wamepokea angalau dozi moja ya chanjo ya Covid-19 katika nchi hiyo ya Afika Mashariki, huku zaidi ya 2,401,926 wakiwa wamepiga dozi kamili ya chanjo hiyo.

Tags