Nov 24, 2021 07:29 UTC
  • Wamorocco waitisha maandamano kulaani safari ya waziri wa vita wa Israel

Wapinzani wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Morocco na Wazayuni wameitisha maandamano ya kulaani safari ya waziri wa vita wa Israel, sambamba na kuanza safari ya waziri huyo wa vita nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Harakati ya Morocco ya Kuunga Mkono Palestina na inayopinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni imewataka wananchi wafanye maandamano mbele ya Bunge la nchi hiyo mjini Rabbat kupinga safari ya waziri wa vita wa Israel, Benny Gantz nchini Morocco. Maandamano hayo yanafanyika leo Jumatano.

Harakati hiyo vile vile imesema kwenye taarifa yake kwamba, inaziomba taasisi zote zinazoguswa na mateso ya Wapalestina pamoja na wanamapambano na wananchi wote wa Morocco washiriki katika maandamano hayo mbele ya Bunge la Morocco mjini Rabbat ili kupinga safari ya Gantz nchini mwao.

Benny Gantz, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Mwezi Disemba 2020, utawala wa Kizayuni wa Israel na Morocco zilitangaza kuanza uhusiano wa kidiplomasia baina yao.

Tangu wakati huo wananchi wa Morocco wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara kuonesha hasira na kuchukizwa kwao na kitendo cha nchi yao cha kujidhalilisha kwa Wazayuni. Wananchi hao wanaamini kuwa kitendo hicho cha Morocco ni usaliti wa wazi wa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

Morocco ilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kufuata mkumbo wa nchi nyingine tatu za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain na Sudan ambazo kabla ya Morocco nazo zilijidhalilishwa kwa Wazayuni kupitia kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel licha ya kuwa kitendo hicho ni usaliti wa wazi wa kadhia ya Palestina.