Nov 24, 2021 07:37 UTC
  • UN: Afrika Magharibi ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watoto wanaotumiwa vitani

Ripoti la Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, kutokana na kuwa katika mazingira ya vita na mapigano ya silaha kwa muda mrefu, watoto wa nchi za magharibi na katikati mwa Afrika ndio wanaounda asilimia kubwa ya watoto wanaotumika vitani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na idadi kubwa ya watoto wanaotumiwa vibaya vitani, nchi za magharibi na katikati mwa Afrika zina idadi kubwa pia ya wahanga wa uhalifu wa kijinsia. Mgogoro wa vita umekuwa ukizidi kuwa mkubwa siku baada ya siku kwa miaka mitano sasa kwenye maeneo hayo ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, watoto zaidi ya 21,000 wamepewa mafunzo ya kijeshi na makundi ya waasi na hata vikosi vya serikali. Zaidi ya hayo, watoto wanaopindukia 2,200 wamekuwa wahanga wa uhalifu wa kijinsia tangu mwaka 2016 hadi hivi sasa. 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, zaidi ya watoto 3,500 wametekwa nyara kwenye maeneo hayo ya magharibi na katikati mwa Afrika na kuyafanya maeneo hayo yawe ya pili kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya utekaji nyara watu ulimwenguni.

Watoto wa magharibi mwa Afrika wanaunda asilimia kubwa ya watoto wanaotumiwa vibaya vitani

 

Tangu mwaka 2005 Umoja wa Mataifa umeanzisha mfumo wa kuchunguza na kutoa ripoti kuhusu uvunjaji mkubwa wa haki za watoto kama vile kuwatumia vitani, kuwateka nyara, kuwabaka, kuvamia maskuli na mahospitali n.k. Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa inaoensha kuwa, kati ya kila kesi nne za uhalifu huo zinazotokea duniani, moja huwa inatokea katika maeneo ya Afrika Magharibi na katikati mwa Afrika.

Ripoti hiyo vile vile imesema, zaidi ya watoto milioni 57 wanahitajia misaada ya kibinadamu, idadi ambayo imeongezeka maradufu mwaka huu kutokana na vita na kuenea magonjwa ya kuambukiza kama corona. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto walioathirika zaidi ni wa nchi za Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Cameroon, Chad, Congo, Mali, Mauritania, na Niger.