Nov 24, 2021 16:19 UTC
  • Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yaunga mkono mwafaka wa kisiasa uliofikiwa nchini Sudan

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema, jumuiya hiyo inaunga mkono makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa nchini Sudan.

Ahmad Abul-Ghaith ametoa msimamo huo katika mazungumzo aliyofanya katika nyakati tofauti kwa njia ya simu na kamanda wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na waziri mkuu wa nchi hiyo Abdalla Hamdok, ambaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25.

Abul Ghaith amesisitiza kwa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iko bega kwa bega na inaiunga mkono serikali na wananchi wa Sudan.

Siku ya Jumapili al-Burhan na Hamdok walisaini hati ya vipengele 14, ambayo moja ya vipengele vyake kinahusu kurejeshwa Abdalla Hamdok kwenye wadhifa wake wa uwaziri mkuu.

Abdalla Hamdok (kushoto) na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

Siku ya Jumatatu, Hamdok alianza kazi tena rasmi kama Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan.

Katika makubaliano hayo imeelezwa pia kwamba, hati ya katiba ya mwaka 2019 ndio marejeo makuu yatakayozingatiwa katika kukamilishia kipindi cha mpito, kurekebsishwa hati hiyo italazimu kufanyike kwa makubaliano, makundi na matabaka yote ya jamii, ukiondoa chama cha taifa kilichovunjwa, yatashirikishwa kwenye mchakato wa kisiasa, wafungwa wote wa kisiasa wataachiwa huru na jeshi la nchi hiyo litakuwa na muundo wa umoja wa kitaifa.../

Tags