Nov 25, 2021 14:05 UTC
  • Jeshi la Burkina Faso lapoteza wanajeshi wake watatu katika vita na magaidi

Jeshi la Burkina Faso limetangaza kuwa wanajeshi wake watatu wameuawa katika operesheni ya kupambana na magaidi iliyopelekea kuuawa wanamgambo 11 wenye silaha kaskazini mwa eneo la Sahel Afrika jana Jumatano.

Taarifa ya jeshi hilo kutoka eneo la Thiou la jimbo la Yatenga imesema kuwa, watu wenye silaha waliwavamia wanajeshi wa serikali katika eneo hilo lakini jeshi lilijihami vizuri na kufanikiwa kuangamiza magaidi 11. Hata hivyo wanajeshi watatu wa serikali wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa.

Shambulio hilo ni moja ya mashambulio matatu ya karibuni kabisa baada ya lile la tarehe 14 mwezi huu wa Novemba ambalo lilipelekea wanajeshi 60 kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakiwemo raia wa kawaida.

Mashambulio hayo ya magaidi yamezusha hasira kubwa za wananchi za kulalamikia wanajeshi wa kigeni hasa wa Ufaransa pamoja na wa serikali na kumtaka Rais Roch Marc Kabore ajiuzulu.

 

Maziko ya wanajeshi waliouawa nchini Burkina Faso

 

Ikumbukwe kuwa siku chache zilizopita waandamanaji wenye hasira nchini Burkina Faso waliufungia njia msafara wa kijeshi wa mkoloni Ufaransa wakati ulipokuwa unaelekea katika nchi jirani ya Niger ikiwa ni kulalalamikia namna mkoloni huyo mkongwe wa Ulaya alivyoshindwa kuwadhaminia usalama wao licha ya kutuma wanajeshi wake katika eneo hilo kwa miaka mingi sasa.

Mamia ya watu wenye hasira walimiminika kwenye njia ulipokuwa unapita msafara wa magari ya wanajeshi wa Ufaransa katika mji wa Kaya. Mmoja wa waandamanaji hao alikuwa amebeba bango lenye maneno yasemayo: "Kaya inasema, wanajeshi wa Ufaransa rudini kwenu." 

Mmoja wa waandamanaji amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema: "Tumewataka wanajeshi wa Ufaransa wafungue magari yao tuone yana nini ndani."