Nov 25, 2021 14:33 UTC
  • Wafanyabiashara ya Utalii Rwanda na Tanzania kuunganishwa

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda imekubaliana kuwaunganisha wafanyabiashara wa Sekta ya Utalii wa nchi hizo ili kukuza utalii.

Hayo yamesemwa leo na Mary Masanja, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yanayoendelea nchini humo.

Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amesema,“Kikubwa tumeweza kukutana na Rais wa wafanyabiashara za kitalii wa hapa nchini Rwanda na tumeomba wafanyabiashara wa huku kushirikiana na wa kwetu kukuza Sekta ya Utalii”

Aidha, Masanja amewataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini mwao.

"Nawaomba Watanzania kwa umoja wetu tuendelee kuwa wazalendo, tuipende nchi yetu na tuendelee kuitangaza nchi yetu kama ambavyo wenzetu wa Rwanda wanavyofanya”, amesisitiza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenzake Paul Kagame wa Rwanda

 

Naye, Naibu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Zephanie Niyonkuru amesema kuwa, Maadhimisho ya Wiki ya Utalii ya Rwanda yamelenga katika kuibua ubunifu katika Sekta ya Utalii nchini humo na kutoa tuzo kwa mshindi.

Kwa upande wake Afisa Masoko Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania, Bernard Mtatiro amesema kupitia Wiki ya Utalii ya Rwanda kwamba, Tanzania itapata fursa ya kutangaza mazao mapya ya utalii kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Kujenga Upya Utalii kwa Ukuaji Endelevu”yamehudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Tanzania, Ghana, Botswana Kenya, Nigeria, Kongo, Afika Kusini, Somalia, Zimbwabwe pamoja na wadau wa utalii kutoka Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.