Nov 26, 2021 07:23 UTC
  • Khalifa Haftar ahukumiwa adhabu ya kifo na mahakama ya kijeshi ya Libya

Mahakama ya kijeshi katika mji wa Misrata nchini Libya imetoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa jenerali mwasi Khalifa Haftar baada ya kumpata na hatia ya kuamuru kushambuliwa Chuo cha Ulinzi wa Anga katika mji huo.

Vyombo vya habari vya Libya vimeripoti kuwa mahakama ya kijeshi ya Misrata imetoa hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Haftar bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.

Adhabu hiyo imetolewa pia kwa askari wengine kadhaa wakiwemo  Abdel Razek al-Nadori, Saqr Jrushi, Abdul Salam al-Hassi, Al-Mabrouk al-Ghazawi, Muhammad Mansour na Saad al-Werfalli.

Kwa mujibu wa chaneli ya Al-Ahrar, mahakama ya kijeshi ya Misrata imetangaza hukumu hiyo baada ya kumshtaki jenerali Khalifa Haftar kuwa alihusika na shambulio dhidi ya makao makuu ya chuo cha ulinzi wa anga mjini humo na kupelekea kuuawa askari mmoja wa chuo hicho.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, mnamo mwaka 2019 ndege za kivita za kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar lilishambulia mara kumi kwa makombora chuo cha ulinzi wa anga cha Misrata.

Matini ya hukumu dhidi ya Haftar imeeleza kuwa ofisi ya mwendesha mashtaka wa jeshi imeiomba idara ya polisi ya jeshi hilo itekeleze hukumu hiyo dhidi ya washtakiwa kulingana na sheria na amri zilizopo.

Hukumu hiyo imetolewa huku Khalifa Haftar akiwa amejitokeza kugombea urais wa Libya katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi ujao wa Desemba. 

Hayo yanajiri huku ikiripotiwa pia kuwa, vyombo vya habari vya Israel vimethibitisha kwamba mwana wa kiume wa Haftar, Saddam Haftar alifanya safari huko na kuomba msaada, mkabala wa ahadi kwamba endapo baba yake atakuwa rais wa Libya, nchi hiyo itafanya mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu wa Kizayuni.../