Nov 26, 2021 10:03 UTC
  • Ethiopia yawafukuza wanadiplomasia wa Ireland

Serikali ya Ethiopia inaoonekana kutekeleza siasa za kulipiza kisasi dhidi ya nchi za Ulaya zinazokosoa siasa zake hasa kuhusu eneo lenye mzozo wa vita la Tigray.

Jumatano serikali ya Addis Ababa ilitoa amri ya kufukuzwa wanadiplomasia wanne kati ya sita wanaohudumu Ethiopia bila kutangaza wazi sababu ya kufanya hivyo. Hata hivyo serikali ya Ireland imesema wanadipoloamsia wake hao wamefukuzwa kutokana na ukosoaji wao dhidi ya serikali ya Addis Ababa kuhusu kadhia ya eneo la Tigray ambapo wamekuwa wakidai kuwa wakazi wa eneo hilo ni wahanga wa siasa za makusudi za serikali ya Ethiopia za kuwatesa kwa njaa.

Ireland ambayo ni mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imekuwa ikikosoa wazi wazi siasa inazozitaja kuwa za ukandamizaji na mateso za serikali ya Ethiopia na mshirika wake Eritrea katika mgogoro wa kibinadamu huko Tigray.

Mgogoro wa kibinadamu unaotokana na mapigano huko Tigray

Simaon Coveney, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland amesema hatua ya Ethiopia kupunguza wanadiplomasia wake nchini humo inatokana na msimamo wa serikali ya Dublin wa kukosoa na kupinga hadharani siasa za serikali ya Addis Ababa katika ngazi za kimataifa na hasa katika Baraza la Usalama kuhusiana na suala zima la Tigray. Amesema nchi yake inaunga mkono kikamilifu juhudi za Umoja wa Afrika za kutatua kwa Amani mgogoro wa Tigray.

Mapigano katika jimbo hilo yamepelekea maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kulazimika kuishi katika mazingira magumu ya kiafya na kukabiliwa na hatari ya baa la njaa. Mapigano hayo yaliibuka Novemba mwaka huu wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmad alipotuma askari kwenda kukandamiza chama kinachotawala jimboni humo cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).