Nov 27, 2021 04:38 UTC
  • Afrika Kusini yaikosoa UK kwa kusimamisha safari za ndege, kisa spishi mpya ya corona

Afrika Kusini imeikosoa vikali serikali ya Uingereza kwa kupiga marufuku raia wa hiyo pamoja na nchi za Botswana, Namibia, Zimbabwe, Lesotho na Eswatini kuingia katika nchi hiyo ya Ulaya, kufuatia kugunduliwa spishi mpya ya corona kwa jina B.1.1.529 katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Katika taarifa jana Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema nchi hiyo ya Ulaya imefanya haraka kuchukua hatua hiyo bila kufanya mazingatio na tafakuri.

Nchi nyingine za Ulaya zinatazamiwa kufuata mkumbo huo na kufuta safari za ndege za kwenda na kutoka katika nchi hizo za eneo la kusini mwa Afrika.

Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limewasifu na kuwapongeza wanasayansi wa Afrika Kusini kwa kugundua haraka spishi hiyo mpya ya virusi vya Corona na kuitaarifu jamii ya kimataifa. Kesi za aina hiyo mpya ya virusi vya corona zimeripotiwa Ubelgiji na ndani ya utawala haramu wa Israel.

Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imejibu kwa njia isiyo ya moja kwa moja hatua ya nchi za Ulaya kuziweka nchi hizo za kusini mwa Afrika kwenye orodha yao nyekundu ya usafiri, kwa kuwataka Waafrika Kusini wote wapige chanjo na kuendelea kufuata kanuni za afya za kujikinga na maradhi hayo.

Taarifa ya Ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa imesisitiza kuwa, kwa kushirikiana na kufuata maagizo ya wataalamu wa afya, Afrika Kusini itaweza kuondokana na taathira hasi za spishi hiyo mpya ya kirusi cha Corona.

Tags