Nov 27, 2021 07:59 UTC
  • Mgombea urais kwa tiketi ya upinzani Sierra Leone kufunguliwa mashtaka ya ufisadi

Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini Sierra Leone imewapata na makosa ya ulaji rushwa maafisa sita akiwemo mwanasiasa wa upinzani maarufu anayetarajiwa kugombea urais kwa tiketi ya vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2023.

Samura Kamara alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha All People's Congress (APC) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018 nchini Sierra Leone.

Vyama vya upinzani vimepanga kumteua mwanasiasa huyo mashuhuri kugombea urais katika uchaguzi ujao.

Wengine waliopatikana na hatia kwa mujibu wa Tume ya Kupambana na Ufisadi ya Sierra Leone ni maafisa wa ngazi ya juu serikalini akiwemo mhasibu wa sasa katika ofisi ya ubalozi wa Sierra Leone katika Umoja wa Mataifa.

Watuhumiwa hao sita wanakabiliwa na mashtaka kadhaa ya ufisadi kuhusiana na wizi wa dola milioni 4.2 zilizokuwa zimepangiwa kutumiwa kwa ukarabati wa ubalozi mdogo wa Sierra Leone, Manhattan.

Rais wa sasa wa Sierra Leone Julius Maada Bio 

 

Kwa mujibu wa tume hiyo, Kamara anakabiliwa na mashtaka mawili yakiwemo matumizi mabaya ya pesa za uma, kiasi cha dola 2,560,000 zilizokuwa zimepangiwa kwa ukarabati wa ubalozi huo mdogo.

Kamara alikuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sierra Leone wakati ufisadi unaodaiwa kufanyika.

Kamara amesema kwamba timu yake ya mawakili inasoma mashtaka ya tume hiyo.

Timu yake ya kampeni imesema kwamba hakufanya kosa lolote ikieleza kwamba “miaka yake 40 katika huduma ya uma, ilikuwa ya uadilifu na hajawahi kuhusishwa ndani na nje ya nchi kuhusiana na kashfa yoyote”.