Nov 27, 2021 12:32 UTC
  • Viongozi wa kisiasa waachiwa huru Sudan baada ya kufanya mgomo wa kususia kula

Wizara ya habari ya Sudan imetangaza kuwa, maafisa kadhaa wa kisiasa wa nchi hiyo wameachiwa huru kutoka jela walizokuwa wakishikiliwa baada ya kufanya mgomo wa kususia kula.

Katika taarifa iliyotoa mapema leo, wizara ya habari ya Sudan imesema, waziri wa zamani wa masuala ya baraza la mawaziri Khalid Omar Yusouf ametolewa jela siku moja baada ya kususia kula.

Mkuu wa zamani wa mkoa wa Khartoum Ayman Nimir, naye pia ameachiwa huru mapema leo.

Hayo yanajiri huku shakhsia mashuhuri wengine kadhaa wa kisiasa wakiwa wangali wako gerezani.

Kwa mujibu wa tamko la chama cha Kongresi cha Sudan, Khalid Omar Yusouf na wafungwa wengine kadhaa waliamua kuanzisha mgomo wa kususia kula kulalamikia kuendelea kuwekwa kizuizini, ilhali kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa kati ya viongozi wa kijeshi na waziri mkuu wa kiraia Abdalla Hamdok, raia wote waliowekwa kizuizini ilipasa waachiwe huru.

Siku ya Jumatatu na Ijumaa iliyopita  pia shakhsia kadhaa wa kisiasa na wanaharakati wa kiraia waliachiwa huru.

Abdalla Hamdok (kulia) na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan baada ya kusaini Mwafaka

Alipohojiwa hivi karibuni na televisheni ya Aljazeera, waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok alisema, amefanya jitihada katika wiki za karibuni kutafuta mwafaka mpya na wanajeshi ili kukomesha umwagaji damu nchini humo.

Mwafaka uliosainiwa siku ya Jumapili iliyopita kati ya Hamdok na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anayeongoza Baraza la Utawala, pamoja na mambo mengine, ulimrejesha tena madarakani waziri mkuu huyo aliyepinduliwa na jeshi sambamba na kusisitiza juu ya kuachiwa huru watu wote waliokamatwa kwa sababu za kisiasa na kuendelezwa mchakato wa mpito kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia nchini Sudan.../

Tags