Nov 27, 2021 13:06 UTC
  • Afrika Kusini: 'Tunaadhibiwa' kwa kugundua spishi mpya ya corona ya Omicron

Afrika Kusini imesema, inahisi "inaadhibiwa" kwa kugundua spishi mpya ya kirusi cha corona aina ya Omicron kutokana na marufuku mbalimbali zilizowekwa zikiwemo za kuzuia wasafiri kutoka nchi za kusini mwa Afrika kuelekea mataifa mengine ya dunia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imeeleza katika taarifa iliyotoa leo kwamba, marufuku za safari za ndege zilizowekwa kufuatia kugunduliwa spishi hiyo ni sawa na kuiadhibu nchi hiyo kwa sababu ya uwezo wake wa juu katika utaalamu wa kijenetiki na kuweza kugundua haraka spishi mpya.

Profesa Tulio de Oliveria, mmoja wa watafiti waliofanya ugunduzi wa aina hiyo mpya ya kirusi cha Corona, naye pia amesema: "Tunaadhibiwa kwa kuwa wawazi".

Takriban visa 100 vimetambuliwa nchini Afrika Kusini, lakini chimbuko lake bado halijajulikana. Hata hivyo nchi mbalimbali duniani zinafunga mipaka yao dhidi ya Afrika Kusini na nchi kadhaa za kusini mwa Afrika. 

Marufuku hizo mpya zimetangazwa kwa ajili ya tahadhari za msambao wa kirusi hicho cha omicron huku Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo pia likitangaza kuwa spishi hiyo ya ugonjwa wa Covid-19 inatia wasiwasi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom

Mbali na Afrika Kusini, spishi hiyo ya corona inayojulikana pia kama B.1.1.529 tayari imeshagunduliwa katika nchi nyingine zisizopungua nne duniani.

Imeelezwa kuwa huenda ikachukua muda wa wiki kadhaa ili kuweza kubaini kama chanjo zinazotumika sasa kwa ajili ya kinga ya ugonjwa wa Covid-19 zina uwezo wa kutosha wa kukabiliana na kirusi hicho kipya au la.

Marekani, Canada na Russia zimeungana na Umoja wa Ulaya na Uingereza kupiga marufuku wasafiri kutoka nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika Kusini yenyewe kuingia katika nchi hizo.../

Tags