Nov 28, 2021 11:58 UTC
  • AU yapinga marufuku ya usafiri kutokana na spishi mpya ya Corona

Umoja wa Afrika umekosoa vikali marufuku za kuzuia wasafiri kutoka nchi za kusini mwa Afrika kuelekea mataifa mengine ya dunia zilizotangazwa na nchi mbalimbali duniani hususan za Magharibi, baada ya kugunduliwa spishi mpya ya kirusi cha corona aina ya Omicron nchini Afrika Kusini.

Dakta  John Nkengasong, Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) amesema historia ya janga la Corona imeonyesha kuwa, marufuku za safari za ndege zina mchango mdogo sana katika kudhibiti msambao wa virusi.

Ameeleza bayana kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kushughulishwa zaidi na suala la kubadilishana data na taarifa za maradhi hayo, sanjari na kuhakikisha kuwa taasisi husika zinaongeza kasi ya kutoa chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.

Afisa huyo wa Afrika CDC ambayo ni taasisi ya AU amesisitiza kuwa, kusimamisha safari za ndege huko nyuma hakukua na matokea yoyote ya maana ya kuzuia msambao wa virusi, na kwamba kinachotakiwa kufanywa ni watu wote kuhakikisha kuwa wanachunga protokali za afya zilizoainishwa, kama kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutumia vieuzi (sanitizer) mara kwa mara.

Kirusi kipya cha Corona

Hapo awali, Afrika Kusini ilizikosoa vikali pia nchi za Ulaya kwa kupiga marufuku safari hizo za ndege za kutoka na kwenda nchini humo, pamoja na nchi za Botswana, Namibia, Zimbabwe, Lesotho na Eswatini, kufuatia kugunduliwa spishi mpya ya Corona.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imeeleza katika taarifa iliyotoa jana kwamba, marufuku za safari za ndege zilizowekwa kufuatia kugunduliwa spishi hiyo ni sawa na kuiadhibu nchi hiyo kwa sababu ya uwezo wake wa juu katika utaalamu wa kijenetiki na kuweza kugundua haraka spishi mpya.

Tags