Nov 29, 2021 15:02 UTC
  • Rais Museveni ahimiza tena kuundwa shirikisho la kisiasa Afrika Mashariki

Kwa mara nyingine tena Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amerejea mwito wake wa kutaka kuundwe shirikisho la kisiasa baina ya nchi za Afrika Mashariki ili kutia nguvu ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi za ukanda huo.

Rais Museveni amesema kuwa, iwapo shirikisho hilo litaundwa, litazalisha soko la pamoja kwa ajili ya mamilioni ya biashara na kutapatikana kambi madhubutu itakayokuwa na nguvu za maamuzi mbele ya washirika wa biashara wa nchi za eneo hilo zikiwemo China, Uingereza na Umoja wa Ulaya. Amesema, shirikisho hilo litatia nguvu ulinzi na usalama kati ya nchi za ukanda huo na hasa zile zinazopakana na nchi kama Somalia, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambazo zina vita.

Vile vile Rais Museveni amewataka wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kutumia vizuri utamaduni wa pamoja wa wananchi wa nchi hizo yakiwemo makabila makubwa yaliyoko mipakani yanayoziunganishwa nchi za ukanda huo kama ambavyo ipo pia fursa ya lugha ya Kiswahii inayoziunganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na kusisitiza kuwa, mambo yote hayo yanalifanya suala la kuwa na shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki kuwa jambo muhimu sana.

 

Amesema: "Mambo yote hayo ya pamoja na ushirikiano wa jadi na wa kale uliopo inabidi utumiwe vizuri kuleta umoja wa kiwango cha juu kabisa katika masuala yote mawili, ya kisiasa na kiuchumi pamoja na soko moja."

Mwaka 2019, Rais Museveni alitoa pendekezo la kuundwa shirikisho la Afrika Mashariki wakati wa mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC uliofanyika mjini Arusha Tanzania. 

Ilikubaliwa kwamba mwaka 2023 uwe wa kuhakikisha shirikisho hilo limeshaundwa lakini hadi hivi sasa mchakato wa kufanikisha suala hilo unakwenda kwa kasi ya kinyonga.