Nov 29, 2021 15:30 UTC
  • Watu 22 wauawa Ituri DRC baada ya kambi ya wakimbizi kushambuliwa tena

Watu wasiopungua 22 wameuawa katika mkoa wa Ituri katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya waasi wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la waasi wa CODECO kuishambulia kambi ya wakimbizi katika mji huo.

Mambo Bapu Mance, Mratibu wa Msalaba Mwekundu katika eneo amesema kuwa, watu 20 waliaga dunia papo hapo kufuatia mashambulio ya waasi wa CODECO huko Ituri huku wawili wengine wakifariki dunia baadaye kutokana na majeraha waliokuwa wameyapata.

Kambi hiyo ya wakimbizi ndio hiyo hiyo ambayo ilishambuliwa na waasi wiki moja iliyopita na kupelekea watu wasiopungua 29 kuuawa.

Wakazi wa vijiji vya mji wa Ituri wanasema umwagaji damu huo umefanyika kwa kiwango hicho cha kuogofya kwa kuwa jeshi la DRC lilichelewa kufika katika maeneo ya tukio lilipoitwa na wananchi.

Waasi wa ADF, moja ya makundi ya waasi yanayofanya harakati mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Wiki iliyopita,  Shirika la Kivu Security Tracker lilitangaza kuwa, kwa akali raia 1,137 wameuawa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri, tangu Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo alipotangaza 'hali ya mzingiro' katika maeneo hayo mawili mwezi Mei.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imetangaza kuwa, hali ya haki za binadamu katika maeneo kadhaa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatia wasiwasi mkubwa.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kukosolewa kutokana na kushindwa kuyatokomeza makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo ambayo yamevuruga kabisa maisha ya wananchi wa maeneo hayo.