Nov 30, 2021 04:36 UTC
  • Chanjo ya corona kuwa lazima nchini Ghana kuanzia mwezi Januari 2022

Serikali ya Ghana imetangaza kuwa, kuanzia mwezi Januari 2022, chanjo ya corona au UVIKO-19 itakuwa jambo la lazima kwa wafanyakazi wote wa sekta za umma, vikosi vya ulinzi na maafisa wa afya.

Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya wa Ghana, Patrick Kuma-Aboagye ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Ghana, kama nchi nyingi za Afrika zimekuwa na kasi ndogo ya kupiga chanjo za UVIKO-19 licha ya kuweko ongezeko la usambazaji wa chanjo hizo katika maeneo mbalimbali. Hadi hivi sasa ni watu milioni 1.4 kati ya raia milioni 30 wa Ghana ndio wamepigwa chanjo kamili za corona.

Daktari Patric amewaambia waandishi wa habari kuwa, serikali ya Ghana itaongeza kasi ya kupiga chanjo za corona kuanzia mwezi ujao wa Disemba na itakapofika mwezi Januari mwakani, wafanyakazi wote wa sekta za umma, vikosi vya kijeshi na wafanyakazi wa afya pamoja na maafisa usalama na wanafunzi wa shule za sekondani, wafanyabiashara na madereva wa umma, wote watatakiwa wawe wamepiga chanjo ndipo wataruhusiwa kufanya kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya nchini Ghana, Dk Patrick Kuma-Aboagye akipigwa chanjo ya corona katika Hospitali ya Ridge mjini Accra.

 

Ushahidi wa kuwa mtu amepiga chanjo utahitajika pia katika vilabu vya usiku, maeneo ya fukweni, viwanja vya michezo na kwenye mikahawa. Hadi hivi sasa ni asilimia 21 tu ya wananchi wa Ghana ndio waliopiga chanjo angalau moja huku asilimia 7 tu wakiwa wamepiga chanjo kamili.

Wizara ya Afya ya Ghana imesema kuwa, takwimu zake zinaonesha kwamba, licha ya kuingizwa idadi kubwa ya chanjo, lakini ni watu milioni 1 na laki nne tu ndio waliopigwa chanjo kamili. Hadi jana jioni, idadi ya wagonjwa wa corona nchini Ghana walikuwa ni watu 131,083 na waliokuwa wamefariki dunia kwa ugonjwa huo walikuwa ni wagonjwa 1,220.