Nov 30, 2021 04:37 UTC
  • Algeria: Tutaendelea kuiunga mkono Palestina hadi ijikomboe kutokana na uvamizi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria ametangaza kuwa, nchi yake itaendelea kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina hadi pale litakapojikomboa kutoka katika ukoloni na uvamizi.

Ramtane Lamamra amesisitiiza kuwa, wananchi wa Algeria wataendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ambao nao kama walivyo watu wengine wana haki ya kujikomboa kunako ukoloni na uvamiz unaowakandamiza.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria ameongeza kuwa, nchi hiyo itaendelea kutoa mchango wake wa kihistoria ambao umejengeka juu ya msingi wa kuwaunga mkono wananchi madhulumu hususan wananchi wa Palestina.

Kadhalika Lamamra amebainisha kuwa, kadhia ya Palestina haifuatiliwi na Algeria kama sera ya kiakili tu, bali kadhia hii ni kitu kisichotenganishika na ufahamu na welewa wa wananchi wa nchi hiyo ambao wanaaamini kuwa, wananchi wa Palestina nao wana haki ya kuishi wakiwa wamejikomboa.

 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria ameongeza kuwa, njama zinazoendeshwa mtawalia dhidi ya nchi yake zenye lengo la kupotosha ule mchango wa kihistoria wa kuiletea Algeria matatizo kutoka nje bila shaka haziwezi kukomeshwa.

Hivi karibuni, Algeria na Afrika Kusini zilitangaza tena msimamo wao wa kupinga utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika (AU).

Algeria, ikishirikiana na nchi zingine 13 wanachama wa Umoja wa Afrika, imetaka kufutwa uwanachama huo wa utawala wa Kizayuni katika AU na kulindwa hadhi na thamani ya asasi hiyo kuu ya bara la Afrika.