Nov 30, 2021 04:45 UTC
  • Maandamano Morocco kupinga uhusiano na Israel

Wananchi wa Morocco wameandamana kupinga hatua ya utawala wa nchi yao kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maandamano hayo yalifanyika Jumapili katika miji 27 kote Morocco kwa mnasaba wa tarehe 29 Novemba  ambayo huadhimishwa kote duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina.

Maandamano hayo yaliandaliwa na Jumuiya ya Morocco ya Kuunga Mkono Palestina ambayo imesema lengo kuu la mijimuiko hiyo lilikuwa ni kubainisha upinzani kwa hatua ya ufalme wa nchi hiyo kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha wananchi waliokuwa na hasira wametaka nchi yao ibatilishe mara moja mapatano yote ambayo imefikia na utawala wa Kizayuni tokea uhusiano wa kawaida uanzishwe bainda ya pande mbili.

Ikumbukwe kuwa mnamo Novemba 23, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benny Gantz alifika Morocco kwa ajili ya safari ya siku mbili. 

Bendera ya utawala wa Israel ikiteketezwa moto katika maandamano Morocco

Pembizoni mwa safari hiyo Morocco na utawala wa Israel zilitiliana saini mapatano katika sekta ya kijeshi.

Ikumbukwe kuwa, nchi nne za Kiarabu za Imarati (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan mwaka uliopita wa 2020 zilisaini hati za makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni, hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa vikali katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Sudan, Morocco na Bahrain zimeendelea kushuhudia maandamano kila leo ya wananchi ya kulaani na kupinga hatua ya nchi zao ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa  Israel. Wananchi waliowengi katika nchi hizo wanasema kuwa, hatua hiyo ni khiyana na usaliti mkubwa kwa wananchi wa Palestina wanaofanyiwa unyama wa kila aina na utawala wa Israel kila uchao.