Nov 30, 2021 08:06 UTC
  • Afrika kupokea msaada wa dozi bilioni 1 za corona kutoka China

Rais Xi Jinping wa China ametangaza kuwa nchi yake itazipa nchi za Afrika msaada wa dozi bilioni 1 za chanjo dhidi ya Covid-19.

Rais wa China ameyasema hayo Jumatatu katika Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika huko Dakar, mji mkuu wa Senegal.

Akihutubu kwa njia ya video katika kikao hicho, Rais wa China Rais Xi ametoa mapendekezo manne kuhusu kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Afrika katika zama mpya, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na janga la COVID-19.

Aidha amesema jumuiya hiyo itazidisha ushirikiano halisi katika masuala ya biashara, uwekezaji, kuondokana na umaskini, uchumi wa kidijitali, ujasiriamali wa vijana wa Afrika na maendeleo ya kampuni ndogo na kukuza maendeleo yasiyoleta uchafuzi wa mazingira, na kulinda usawa na haki.

Rais wa China  Xi Jinping akihutubia mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) 

Rais Xi amesema, kufuatia mpango wa kwanza wa miaka mitatu wa “Malengo ya Mwaka 2035 ya Ushirikiano kati ya China na Afrika”, China itashirikiana kwa karibu na Afrika kutekeleza kwa pamoja “miradi tisa,” ambayo ni China kusaidia Afrika kukabiliana na janga la COVID-19, kuisaidia Afrika kupunguza umaskini na kuendeleza kilimo, kukuza biashara kati ya China na Afrika na kuongeza uagizaji wa bidhaa za Afrika hadi kufikia dola bilioni 300 za Kimarekani katika miaka mitatu ijayo.

Hali kadhalika amesisitiza kuhusu kuongeza uwekezaji barani Afrika, kuhimiza uvumbuzi wa kidijitali barani Afrika, kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira, kuisaidia Afrika kujenga uwezo, kuhimiza mawasiliano ya ustaarabu na watu, na kuisaidia Afrika kuimarisha amani na usalama.