Nov 30, 2021 10:55 UTC
  • Kushtadi mgogoro wa Ethiopia; indhari ya hatari ya kugawanywa nchi na kudhibitiwa mji mkuu

Mgogoro wa Ethiopia umechukua wigo mpana zaidi kiasi kwamba, akthari ya weledi wa mambo wa mambo wanatahadharisha juu ya uwezekano wa kutekwa na kuangukia mikononi mwa waasi mji mkuu Addis Ababa na kuenea vita vya ndani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Machafuko na mapigano yalianzia katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.  Japokuwa mivutano na vita baina ya jeshi la serikali kuu na wakazi wa Tigray vina historia kongwe, lakini mapigano mapya yaliyozuka kuanzia Novemba mwaka jana (2020) ni makubwa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Mapigano hayo yalianza baada ya viongozi wa jimbo la Tigray kufanya mambo kinyume na matakwa ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuhusiana na uchaguzi. Asilimia 6 ya wakazi wa jimbo la Tigray ambao ni jamii ya waliowachache nchini Ethiopia inaamini kuwa, serikali kuu ya Addis Ababa inapuuza maslahi ya wakazi wa jimbo hilo.

Dhana hii ndio iliyopelekea kuimarika fikra ya kupigania kujitenga na Ethiopia jimbo la Tigray. Hii ni katika hali ambayo, kwa mtazamo wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed ni kuwa, serikali ya sasa ya jimbo hilo siyo halali na inatumia mabavu ili iwe na satua na ushawishi katika eneo hilo. Hali hiyo ndio iliyolisukuma jeshi la serikali kuu na inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuanzisha vita dhidi ya Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF). Awali Abiy Ahmed aliahidi kwamba, operesheni hiyo itadumu kwa muda mfupi.

Mashambulio ya anga ya jeshi la Ethiopia dhidi ya jimbo la Tigray

 

Lakini kinyume na matarajio yake, vita hivyo siyo tu kwamba, vimeendelea kushuhudiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, bali vimeshtadi na kutishia kuigawa nchi.

Utumiaji mabavu na vita vinaonekana kuchukua wigo mpana hasa baada ya kusambaa katika maeneo mbalimbali ya Ethiopia, kiasi kwamba, hivi karibuni Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alizituhumu pande zote mbili nchini Ethiopia kwamba, zimekiuka haki za binadamu na hata kutenda jinai dhidi ya binadamu. Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamesonga mbele na hivi sasa wapo umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu Addis Ababa.

Kuendelea kusonga mbele wapiganaji wa harakati hiyo, kumemfanya Waziri Mkuu Abiy Ahmed akabidhi majukumu ya uongozi wa nchi kwa naibu wake na yeye kuchukua usukukani wa kuongoza operesheni za kijeshi vitani dhidi ya wanaharakati wa TPLF.

Vita vimeshadidi na kupamba moto nchini Ethiopia katika hali ambayo, Tomson Phiri, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ametahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mauaji kizazi kwa maana halisi ya neno huko kaskazini mwa Ethiopia na kutangaza kuwa, zaidi ya watu milioni 9 nchini Ethiopia wanaishi katika hali na mazingira mabaya mno.

Wapiganaji wa harakati ya TPLF

 

Ethiopia ambayo ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika baada ya Nigeria, inahesabiwa kuwa moja ya nchi muhimu zaidi katika eneo la Pembe ya Afrika.

Kijiografia Pembe ya Afrika inajumuisha nchi za Somalia, Ethiopia, Eritrea na Djibouti. Umuhimu wa kijiopolitiki na kijiostratejia wa Pembe ya Afrika  kutokana na kuwa na mpaka wa pamoja na Bahari ya Hindi, Ghuba ya Aden, Lango Bahari la Bab al-Mandab na Bahari Nyekundu umelifanya eneo hilo kuwa na umuhimu maalumu katika nidhamu ya kimataifa. Kuwa na sifa hizi eneo hili, kumelifanya daima liwe ni lenye kuzingatiwa na wachezaji wa siasa za eneo na nje ya eneo ambao wamekuwa wakifanya kila wawezalo kupenya na kuwa na satua katika eneo hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni pia, utawala haramu wa Kizayuni wa Kizayuni wa Israel ambao siasa zake zimegonga mwamba katika maeneo mengine ya dunia umeelekeza harakati zake barani Afrika, na Marekani ambayo ni muitifaki na muungaji mkono mkuu wa Israel imekuwa na uwepo mkubwa katika mataifa ambayo utawala huo ghasibu una satua na ushawishi ikiwemo Ethiopia.

Wakimbizi katika jimbo la Tigray

 

Kutekelezwa mradi wa ujenzi wa Bwawa na al-Nahdha ambao kivitendo una taathira kwa uchumi na siasa za nchi kadhaa muhimu za eneo kama Misri na ambao unasimamiwa na mashirika ya Israel ni moja ya mifano hiyo, jambo ambalo limeifanya Washington nayo iwe na uwepo mkubwa katika nchi hiyo. Aidha kushadidi mgogoro wa Tigray kumemfanya Rais Joe Biden wa Marekani achukue uamuzi wa kuiwekee vikwazo Ethiopia.

Vyovyote itakavyokuwa, kushadidi mapigano na vita nchini Ethiopia kumeifanya nchi hiyo iingie katika hatua mpya ambayo huenda ikapelekea kuibuka vita vya ndani kati nchi hiyo na hivyo kuigawa nchi, hali ambayo kuja kuondokana nayo, kitakuwa kibarua kigumu kitakachoambatana na kulipa gharama nyingi za mali na roho za watu.

Tags