Nov 30, 2021 10:56 UTC
  • Wakimbizi 886 waokolewa katika fukwe ya Libya kwenye kipindi cha wiki moja

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji limesema kuwa, wahamiaji 886 wameokolewa na kurudishwa nchini Libya katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imesema: "Katika kipindi cha kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 27 mwezi huu wa Novemba, wahamiaji 886 wameokolewa baharini na kurejeshwa nchini Libya."

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 hadi hivi sasa, wahamiaji 30,990 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameokolewa, 506 wamekufa maji na wengine 807 wamepotea na hawajapatikana hadi hivi sasa katika ufukwe wa Libya unaopakana na Bahari ya Mediterranian.

Wakimbizi wengi ambao wengi wao ni kutoka nchi za Afrika wanapenda kutumia Bahari ya Mediterranean kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya maisha mazuri. Libya imekuwa kimbilio kubwa la wahamiaji hao haramu kutokana na kutokuweko serikali kuu yenye nguvu tangu alipopinduliwa kiongozi wa zamani wa Libya, Muhammad Gaddari mwaka 2011.

Operesheni ya kuokoa wahamiaji haramu nchini Libya

 

Pamoja na hayo si wakimbizi wa nchi za Afrika tu wanaopenda kutumia ardhi ya Libya kuelekea barani Ulaya. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba, Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) lilitangaza kuwa limewarejesha nyumbani wahamiaji 140 wa Bangladesh walioingia nchini Libya kinyume cha sheria.

Katika taarifa yake hiyo, IOM lilisema kuwa, wahamiaji haramu kutoka Bangladesh ambao tisa kati yao walikuwa wagonjwa, wamesaidiwa kurudi nchini kwao kwa hiari ikiwa ni sehemu ya mpango maalumu wa kuwarejesha nyumbani kwa hiari wahamiaji haramu unaosimamiwa na IOM pamoja na Mpango wa Kurejea Nyumbani kwa Hiari ujulikanao kwa kivupi kwa jina la VHR.