Nov 30, 2021 11:31 UTC
  • Jeshi la Uganda lafanya mashambulio ya anga dhidi ya waasi wa ADF huko DRC

Jeshi la Uganda limeanzisha mashambulizi ya pamoja ya anga na ardhini dhidi ya kundi la waasi la Allied Democratic Forces -ADF, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Uganda Brigedia Jenerali Flavia Byekwaso amethibitisha hayo kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa Twitter.

Brigedia Jenerali Flavia Byekwaso ameongeza kuwa, operesheni hizo zilifanywa na washirika wa Congo, dhidi ya kambi za waasi wa ADF, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu maeneo ambayo mashambulizi hayo yamefanywa.

Serikali ya Uganda imekuwa ikiwalaumu waasi wa ADF, ambao wametangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la Daesh kwamba, limehatarisha usalama wan chi hiyo hasa baada ya milipuko kadhaa ya hivi karibuni katika mji mkuu Kampala.

Waasi wa ADF wanaoebdesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Kundi la ADF lilitangaza kuhusika na shambulio la bomu lililotokea mwezi uliopita  wa Oktoba karibu na mkahawa maarufu wa Kawempe jijini Kampala.

Kwa muda mrefu, kundi hilo la kigaidi limekuwa likipinga utawala wa Rais Yoweri Museveni, kiongozi wa muda mrefu wa Uganda na muitifaki wa kiusalama wa Marekani, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kiafrika kutuma askari wa kulinda amani nchini Somalia ili kuihami serikali kuu ya nchi hiyo dhidi ya hujuma za kundi la kigaidi la al-Shabab.

Wanamgambo wa ADF wanahesabiwa kuwa ni waasi makatili zaidi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Majimbo ya Kivu Kaskaizni na Ituri yamekuwa yakishuhudia mashabulizi ya mara kwa mara ya kikatili ya waasi hao.