Nov 30, 2021 11:58 UTC
  • Kuendelea maandamano ya Wasudan mjini Khartoum

Wananchi wa Sudan wanaendelea kufanya maandamano kulalamikia mapatano ya kisiasa yaliyofikiwa nchini humo pamoja na kutaka serikali ya kiraia iundwe haraka nchini.

Kamati za mapambano na vyama vya wafanyakazi vimeitisha maandamano makubwa leo Jumanne kwa ajili ya kufuatiliwa matakwa ya wananchi kutoka kwa serikali inayodhibitiwa na wanajeshi.

Wakati huo huo, Stephane Dujarric, Msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika kikao kwamba kwa mtazamo wa umoja huo, kurejea madarakani Waziri Mkuu Abdalla Hamdok hakujamaliza mgogoro wa Sudan bali kumepunguza tu makali ya mgogoro ambao huenda ungekuwa mkubwa zaidi.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaamini kwamba Sudan inahitajia kipindi cha mpito ambacho kitaandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini.

Abdalla Hamdok (kushoto) na al-Burhan

Tangu Oktoba 25 Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano ya wananchi ambao wanapinga hatua ya Abdulafattah al-Burhan, kamanda mkuu wa jeshi la Sudan ya kuvunjilia mbali Baraza la Utawala wa Mpito na Baraza la Mawaziri na kisha kumtia nguvuni waziri mkuu na kutangaza hali ya hatari nchini.

Licha ya kwamba al-Burhan na Hamdok tarehe 21 mwezi huu walitia saini mapatano ya kisiasa ambayo yanatazamiwa kupelekea kuundwa serikali mpya na kuendeleza mwenendo wa kurudishwa demokrasia nchini lakini makundi ya kisiasa na kiraia ya nchi hiyo yanapinga mapatano hayo yakiyataja kuwa ni juhudi za kuhalalisha mapainduzi ya kijeshi yaliyofanywa na wananchi nchini.

Wasudan wanasema wataendeleza maandamano yao dhidi ya wanajeshi hadi pale serikali kamili ya kiraia itakapoundwa nchini.

Tags