Nov 30, 2021 12:01 UTC
  • Jeshi lamwachilia huru Rais Alpha Conde na kumpeleka nyumbani kwake Conakry

Jeshi la Guinea limetangaza kuwa limemwachilia huru Rais Alpha Conde aliyepinduliwa na jeshi hilo na lilimpeleka nyumbani kwake jana Jumatatu, katika viunga vya mji mkuu Conakry.

Hatua hiyo imekuja baada ya jeshi hilo kumuweka korokoroni Conde na kumkatia mawasiliano yote na watu wa nje kwa miezi kadhaa. Alpha Conde 83, ameitawala Guinea kwa muda wa miaka 11 kabla ya kupinduliwa na jeshi tarehe 5 Septemba mwaka huu. 

Katika taarifa hiyo ya jeshi iliyotangawza na televisheni ya taifa, wanajeshi waliofanya mapinduzi wamesema kuwa, Conde hivi sasa yuko kwa mkewe Hadja Djene Kaba Conde katika viunga vya mji wa Conakry. Pamoja na hayo taarifa hiyo haikusema iwapo atakuwa chini ya kifungo cha nyumbani au la.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS imeiwekea vikwazo Guinea na kila mwanajeshi aliyeshiriki kwenye mapinduzi, ikishinikiza kuachiliwa huru Alpha Conde bila ya masharti yoyote.

Kanali Mamady Doumbouye aliyefanya mapiduzi kijeshi Guinea Conakry na kujitangaza rais wa mpito

 

Jumuiya hiyo imesimamisha uanachama wa Guinea na kushinikiza kufanyika uchaguzi katika kipindi cha miezi sita ijayo. Ikumbukwe kuwa, Kanali Mamady Doumbouye aliyeongoza mapinduzi hayo, aliapishwa kuwa rais wa mpito wa Guinea, mwezi uliopita wa Oktoba.

Licha ya Kanali Doumbouya kuahidi kurejesha utawala wa raia na kuitisha uchaguzi huru kwa haraka, lakini hadi hivi sasa amekataa kutangaza tarehe yoyote ya kufanyika jambo hilo.

Kanali huyo wa kijeshi aliyepewa mafunzo na mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa anadai kuwa amelazimika kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa sababu Rais Alpha Conde alikuwa mbadhirifu na alihodhi peke yake madaraka yote ya nchi.