Dec 01, 2021 03:43 UTC
  • Al-Shabaab yashambulia askari wa Ethiopia, uwanja wa ndege Somalia

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limeshambulia uwanja wa ndege na kambi ya kijeshi ya askari wa Ethiopia katika mji wa Baidoa, ulioko kusini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, kwa akali askari mmoja ameuawa katika shambulio la kwanza lililolenga kambi ya jeshi la Ethiopia katika eneo la Suuqa Hoolaha jijini Baidoa, huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Abdi Ali Mohamud, afisa wa polisi jijini Baidoa amesema wanamgambo wa al-Shabaab wametumia silaha nzito katika shambulizi hilo dhidi ya askari wa Ethiopia, ambao ni sehemu ya wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).

Wakati huo huo, raia mmoja ameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulio jingine dhidi ya uwanja wa ndege jijini Baidoa, yapata kilomita 243 kusini magharibi mwa Mogadishu. Baidoa ndio mji mkubwa zaidi katika jimbo la Kusini Magharibi nchini Somalia.

Askari wa AMISOM nchini Somalia

Hili ni shambulio la pili la genge la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda jijini Baidoa, tangu uchaguzi wa Bunge katika eneo hilo uanze mapema wiki hii.

Jeshi la Somalia kwa kusaidiwa na kikosi cha AMISOM lilifanikiwa kuwafurusha magaidi wa al-Shabaab katika mji mkuu Mogadishu, mwezi Agosti 2011, lakini wanamgambo hao wanadhibiti maeneo ya vijijini ya kusini na katikati mwa Somalia na wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine.

 

Tags