Dec 01, 2021 08:21 UTC
  • Wasudan waandamana kupinga utawala wa wanajeshi

Wananchi wa Sudan wangali wanaendeleza maandamano ya kupinga mapatano ya kisiasa yaliyofikiwa karibuni kati ya wanajeshi na Abdalla Hamdok, ili kumrejesha kiongozi huyo katika nafasi yake ya Waziri Mkuu.

Wananchi Jumanne alasiri waliandamana katika karibu miji yote mikubwa ya Sudan kulaani mapatano hayo yaliyotiwa saini kati ya Abdulfattah al-Burhan, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan na Abdalla Hamdok, ili kumrejeshea kiti chake cha Waziri Mkuu.

Huku wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa jumbe tofauti za kulaani mapatano hayo ya kisiasa yanayotiliwa shaka, waandamanaji walisisitiza kuwa hawatakubali mapatano  ambayo yatawatenga raia na kutowashirikisha katika mwenendo wa uendeshaji wa mambo ya nchi yao.

Wengi wa waandamanaji wanapinga vikali suala la kushirikishwa wanajeshi katika masuala ya uongozi wa nchi na kwamba badala yake wanapasa kuandaa uwanja wa kufanyika uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo.

Abdalla Hamdok

Askari jeshi na polisi walitumia risasi hai na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji ambapo wengi wao walijeruhiwa.

Abdulfattah al-Buran na Abdalla Hamdok Novemba 21 walitiliana saini mapatano ya kisiasa ya kumrejesha madarakani waziri mkuu huyo lakini wananchi wanayapinga na kuyataja kuwa yanayolenga kuhalalisha mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi kwa lengo la kuzuia mwenendo wa demokrasia nchini.

Inadaiwa kuwa mapatano hayo yalifikiwa kwa msingi wa katiba ya Sudan ya mwaka 2019 ambapo baadhi ya vipengee vyake vinasisitiza kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa na kubuniwa jeshi moja na imara la Sudan.

Tags