Dec 01, 2021 11:36 UTC
  • Jeshi la Ethiopia lachukua miji iliyokuwa imetekwa na TPLF

Serikali ya Ethiopia imesema jeshi lake limefanikiwa kuchukua udhibti wa mji wa Shewa Robit, mji ulio kilomita 220 kutoka mji mkuu Addis Ababa. Mji huo muhimu ulikuwa umetekwa na waasi wa kundi la TPLF.

Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu ametangaza kuwa Shewa Robit ni kati ya miji kadhaa midogo midogo ambayo imerejea mikononi mwa serikali na vikosi vya kieneo ambavyo vinamuunga mkono waziri mkuu Abiy Ahmed ambaye wiki iliyopita alielekea katika medani ya vita kuongoza mapambano ya kukabiliana na waasi wa TPLF waliokuwa wanatishia kuuteka mji mkuu, Addis Ababa.

Legesse amesema: “Katika medani ya vita eneo la Shewa miji ya Mezezo, Molale, Shewa Robit na Rasa imekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa TPLF.” Aidha amesema jeshi la serikali linakaribia kudhibiti tena eneo la Dessie na Lalibela, ambalo liko katika orodha ya UNESCO ya turathi za dunia, ambalo lilitekwa na waasi wa TPLF mwezi Agosti.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Japokuwa mivutano na vita baina ya jeshi la serikali kuu na waasi Tigray vimekuwepo kwa muda mrefu, lakini mapigano mapya yaliyozuka kuanzia Novemba mwaka jana (2020) ni makubwa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Mapigano hayo yalianza baada ya viongozi wa jimbo la Tigray kufanya mambo kinyume na matakwa ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuhusiana na uchaguzi.