Dec 01, 2021 11:57 UTC
  • Watu 29, wakiwemo watoto, wapoteza maisha katika ajali ya boti Nigeria

Watu 29, wengi wakiwa ni watoto, wamepoteza maisha baada ya boti yao kuzama Nigeria katika Mto Bagwai jimboni Kano kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Msemaji wa kitengo cha zimamoto jimboni Kano Saminu Abdullahi amesema ajali hiyo ilitokea Jumanne usiku.

Akizungumza Jumatano, Abdullahi amesema wamepata miili 29 na kuwaokoa abiria saba huku jitihada zikiendelea kwa ajili ya kutafuta miili 13. Amesema boti hiyo inaruhusiwa kubeba abiria 12 watu wazima lakini watoto wengi walijazwa humo na hivyo kusababisha ajali.

Watoto hao walikuwa wanatoka kijiji cha Badau kuelekea mji Bagwai kuhudhuria hafla ya kidini wakati ajali hiyo ilipotokea.

Ajali za boti hujiri mara kwa mara Nigeria kutokana na kupakiwa abiria kupita kiasi, na wakati mwingine kutokana na hali mbaya ya hewa na ukosefu wa ukarabati wa mara kwa mara.

Mwezi jana wasichana saba walipoteza maisha katika jimbo jirani la Jigawa baada ya boti yao kuzama kwenye mto. Aidha Juni watu 13 walipoteza maisha jimboni sokoto baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuelekea harusi ilipozama.