Dec 02, 2021 03:00 UTC
  • Makumi ya watu watekwa nyara jirani na Cabo Delgado nchini Msumbiji

Watu wenye silaha wamewateka nyara zaidi ya vijana 100 kutoka kijiji cha Naulala katika Mkoa wa Niassa kaskazini mwa Msumbiji.

Mji wa Niassa unapakana na jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji ambalo limekuwa katikak vita na makundi ya wanamgambo tangu Oktoba 2017.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kundi la watu wenye silaha limewateka nyara vijana zaidi ya 100 na kuchoma makazi na vibanda katika kijiji cha Naulala, Mkoa wa Niassa, kaskazini mwa Msumbiji.

Vyombo vya habari vya Msumbiji hapo awali viliripoti msururu wa mashambulizi kwenye mpaka wa Cabo Delgado na Niassa ambapo takriban maafisa watano wa polisi waliuawa.

Jimbo tajiri kwa nishati ya gesi la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na machafuko na hujuma za wanamgambo wenye mfungamano na kundi9 la kigaidi la Daesh tangu mwishoni mwa mwaka 2017. Watu wasiopungua 3,000 wameuliuwa hadi sasa katika hujuma za wanamgambo hao na wengine laki nane wamelazimika kuhama makazi yao

Wanamgambo wa Msumbiji wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh

 

Machi mwaka huu, magaidi nchini Msumbiji waliuteka mji wa Palma wa kaskazini mwa nchi hiyo ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania, na kuua makumi ya watu na kuwalazimisha kuwa wakimbizi watu wengine zaidi ya 50,000. Eneo hilo limekumbwa na uasi baada ya kuanza mradi wa gesi wa dola bilioni 20.

Mwezi Julai mwaka huu, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC ilianza kutuma wanajeshi wake kulisaidia jeshi la Msumbiji kupambana na magaidi waliojizatiti kaskazini mwa nchi hiyo.