Dec 03, 2021 04:25 UTC
  • Afrika CDC: Dunia isibabaike kutokana na kirusi cha Omicron

Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuwa watulivu na iache kubabaika kutokana na kugunduliwa spishi mpya ya kirusi cha corona aina ya Omicron.

Dakta  John Nkengasong, mkuu wa Africa CDC ambayo ni taasisi ya Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa, "Sote tuna wasi wasi, lakini hali hii inaweza kudhibitiwa. Hakuna haja ya mfadhaiko, kinachotakiwa kufanywa ni watu wote kuhakikisha kuwa wanachunga protokali za afya zilizoainishwa, kama kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutumia vieuzi (sanitizer) mara kwa mara."

Afisa huyo wa Afrika CDC ameongeza kuwa, taasisi hiyo kwa muda mrefu imejiandaa kuhusu uwezekano wa kuibuka spishi mpya, na kwamba hili ni jambo ambalo lilitarajiwa.

Amesema tayari kirusi cha Omicron kimesharipotiwa katika nchi nne za Afrika, ambazo ni Afrika Kusini, Ghana, Nigeria na Botswana, akisisitiza kuwa bara hilo linakabiliwa na wimbi la nne la msambao wa virusi vya Corona.

Mkuu wa Afrika CDC, Dakta Nkengasong

Hivi karibuni pia, Dakta Nkengasong alikosoa vikali marufuku za kuzuia wasafiri kutoka nchi za kusini mwa Afrika kuelekea mataifa mengine ya dunia zilizotangazwa na nchi mbalimbali duniani hususan za Magharibi, baada ya kugunduliwa spishi hiyo mpya.

Juzi Jumatano pia, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Moussa Faki Mahamat alisema marufuku za safari za ndege zilizotangazwa na baadhi ya nchi dhidi ya nchi za kusini mwa Afrika hazina mantiki, na kwamba historia ya janga la Corona imeonyesha kuwa, marufuku hizo zina mchango mdogo sana katika kudhibiti msambao wa virusi.

Tags