Dec 03, 2021 04:33 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa kisiasa Tunisia

Licha ya mgogoro wa kisiasa wa Tunisia kuendela kwa miezi kadhaa sambamba na kufanyika juhudi za kujaribu kuumaliza, lakini juhudi hizo zimeshindwa kuzaa matunda.

Katika uwanja huo, Rais Kais Saied wa Tunisia ameeleza kusikitishwa kwake na vyombo vya mahakama katika kuchelewesha uchunguzi wa ripoti zinazohusiana na ukiukaji uliofanyika katika mwenendo wa uchaguzi mkuu uliopita na kutaka njia mbadala zitafutwe kwa ajili ya kushughulikia haraka suala hilo.

Ni wazi kuwa takwa hilo la Rais Kais Saied limewakasirisha wapinzani wake. Mjadala kuhusu mfumo wa mahakama nchini Tunisia limebadilika kuwa uwanja wa malumbano makali ya kisiasa kati ya Kais Saied na wapinzani wake. Huku Rais Saied akisisitiza kupambana na ufisadi katika mfumo huo, wapinzani wanasema vyombo vya mahakama vinapasa kujiepusha kusukumwa katika malumbano na tofauti za kisiasa.

Muhammad Buaud mwandishi magazeti wa Tunisia anasema: Uamuzi mzuri kwa rais wa nchi ni kuwa badala ya kutumia dikrii za rais au mbinu nyingine katika kuingilia masuala ya vyombo vya mahakama na hivyo kupunguza itibari yake ya kisheria, anapasa kutumia njia tofauti kushawishi na kuukinaisha mfumo wa mahakama uharakishe juhudi za kuchunguza masuala kama hayo.

Kais Saied

Miezi kadhaa iliyopita, Rais Kais Saied alivunja bunge la na kuwafukuza kazi maafisa wengi wa serikali hatua ambayo ilitajwa na baadhi ya vyama vya siasa vya Tunisia kuwa mapinduzi. Hatua yake hiyo ambayo ilipelekea kucheleweshwa kufunguliwa bunge na kuakhirishwa kuteuliwa waziri mkuu ilichochea maandamano makubwa ya Watunisia ambao wanahofia kupotea matunda ya mapambano yao ya 2011 na vilevile kusambaratishwa mwenendo wa demokrasia nchini. Mashinikizo ya kijamii ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi ya Rais Kais Saied hatimaye yalimlazimu kumteua waziri mkuu na kuarifishwa baraza jipya la mawaziri.

Najla Bouden Ramadan mara tu baada ya kuteuliwa na Rais Saied kuwa waziri mkuu, alitangaza kuwa jukumu lake la kwanza lingekuwa ni kurejesha imani ya Watunisia kwa serikali na kuvutia uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kwa serikali hiyo. Licha ya serikali hiyo kuwa madarakani kwa miezi kadhaa sasa lakini bado kuna malalamiko na ukosoaji mkubwa wa wananchi kwa utendahi wa Rais Kais Saied.

Vyama vya upinzani vinamkosoa kuwa ameamua kuingilia kinyume cha katiba utendaji wa vyombo vya mahakama kwa ajili ya kudhamini maslahi yake ya kisiasa nchini. Vinasema licha ya nara za rais huyo katika miezi ya karibuni, lakini hajafanya lolote la maana katika kupambana na ufisadi na ugaidi bali amekuwa akitumia wakati wake mwingi kufuatilia malengo ya kisiasa na kuimarisha nafasi ya kushinda katika uchaguzi ujao. Chama kikuu cha upinzani nchini Tunisa, an-Nahdha pia kimetahadharisha kuhusu siasa za Kais Saied na kusema huenda zikaitumbukiza nchi katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na hatimaye kusambaratisha mkondo wa kurejeshwa demokrasia nchini.

Najla Bouden Ramadan

Malumbano ya kisiasa yanaendelea huko Tunisia katika hali ambayo mgogoro wa kiuchumi umeibua makelele na malalamiko mengi ya Watunisia na wakati huo huo kufungua mlango wa nchi za kigeni na hasa Marekani, kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Suala hilo linakosolewa na wanasiasa na wapinzani wa serikali ambao wanasema hawatakubali nchi za kigeni kuruhusiwa na serikali ya Rais Kais Saied kuingilia masuala ya ndani ya Watunisia.

Kwa kuzingatia hayo na kuendelea hatua za Rais Saied kusukuma mbele siasa zake bila kujali matakwa ya vyama vya upinzani na wananchi wa Tunisia, ni wazi kuwa huenda nchi hiyo ikashuhudia wimbi jipya la malalamiko na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali katika siku zijazo.

Tags