Dec 03, 2021 07:50 UTC
  • Mamilioni ya dola yatengwa kwa ajili ya chanjo ya malaria Afrika

Muungano wa Chanjo Ulimwenguni (GAVI) umetangaza kuwa, bodi yake imeidhinisha kiasi cha dola milioni 155.7 kwa ajili ya zoezi la utoaji wa chajo za kwanza za ugonjwa wa malaria kwa watoto kwenye mataifa yaliyoko chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.

Jose Manuel Barroso Mwenyekiti wa Muungano wa Chanjo Ulimwenguni (GAVI) ameonyesha kufurahishwa na hatua ya bodi yake akiongeza kwamba, hilo limewezekana kupitia juhudi za pamoja za jamii ya kimataifa ya afya, na kwamba zoezi hilo litakapoanza, basi litaokoa mamilioni ya maisha ya watoto

Fedha zilizoidhinishwa zitatumika kwa ajili ya kuagiza na kusafirisha chanjo hizo pamoja na hatua nyingine za kuzuia maambukizi kama vile neti za mbu. Malaria huua watu wapatao 500,000 kila mwaka ulimwenguni huku nusu yao wakiwa ni watoto wadogo wa bara la Afrika.

 

Wataalamu wanasema kuwa, chanjo hii ya malaria iliyopasishwa siyo kwamba, haina mapungufu, lakini inatarajiwa kusaidia pakubwa juhudi za kupambana na malaria.

Mwezi Aprili mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilizindua mpango kabambe wenye lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria katika nchi 25 duniani ifikapo mwaka 2025. Tangu mwaka wa 2019, nchi tatu za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ghana, Kenya na Malawi, zilianza kutumia chanjo hiyo katika maeneo yaliyochaguliwa ambapo maambukizi ya malaria yamekuwa yakiongezeka.

Chanjo ya ugonjwa ya ugonjwa wa malaria iitwayo "RTS, S/AS01" iliyoidhinishwa na kupendekezwa na Shirika la Afya Duniani imefanyiwa utafiti kwa zaidi ya miaka 30 na inatarajiwa kubadilisha historia ya afya ya umma.