Dec 03, 2021 10:49 UTC
  • Mahakama yaruhusu mwana wa Gaddafi agombee urais, vituo vya kura vyashambuliwa Libya

Mahakama moja ya kusini mwa Libya jana ilitoa idhini kwa Seif al Islam, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi agombee urais katika uchaguzi wa tarehe 24 mwezi huu wa Disemba. Mahakama ya Sebha imesikiliza kesi iliyofunguliwa na Seif al Islam Gaddafi ya kupinga uamuzi wa tume ya uchaguzi ya Libya wa kumkatalia kugombea urais nchini humo mwezi uliopita. 

Huku hayo yakiripotiwan, tume hiyo ya taifa ya uchaguzi ya Libya (HNEC) ilisema jana Alkhamisi kuwa, vituo vyake vinne vya uchaguzi vimeshambuliwa na watu wenye silaha waliokuwa wamevaa nguvo za raia. Kwa mujibu wa Said Al-Qasabi, mkuu wa kitengo cha operesheni maalumu cha tume hiyo ya uchaguzi amesema, mashambulio hayo yametokea kwenye mji Sebha wa kusini mwa Libya.

Tume ya taifa ya uchaguzi ya Libya ilitegemea kifungu cha sheria ya uchaguzi kinachowazuia watu kugombea urais kama wamewahi kushtakiwa kwa uhalifu na lazima wakabidhi rekodi inayowasafisha na uhalifu. 

Mwishoni mwa mwezi ulioisha wa Novemba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya iliwakatalia wagombea 25 akiwemo Saif al Islam Gaddafi mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi kugombea uchaguzi ujao wa rais nchini humo.

Seif al Islam Gaddafi na jenerali muasi Khalifa Haftar

 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya ilitangazapia  kuwa imethibitisha katika orodha ya kwanza  majina ya watu 73 wanaostahiki kugombea katika uchaguzi wa rais akiwemo Khalifa Haftar Kamanda wa kundi la wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya. 

Hata hivyo muda mfupi baadaye, mahakama ya kijeshi katika mji wa Misrata nchini Libya ilitoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa jenerali muasi Khalifa Haftar baada ya kumpata na hatia ya kuamuru kushambuliwa Chuo cha Jeshi la Anga cha mji huo.

Vyombo vya habari vya Libya viliripoti kuwa mahakama ya kijeshi ya Misrata imetoa hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Haftar bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani. Adhabu hiyo ilitolewa pia kwa askari wengine kadhaa.