Dec 04, 2021 02:36 UTC
  • UN na AU zatoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Ethiopia, onyo la kukaririwa hali ya Kabul latolewa

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimetoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Ethiopia, huku afisa wa Umoja wa Mataifa akionya dhidi ya kukaririwa hali iliyoshudiwa Kabul nchini Afghanistan baada ya Taliban kuidhibiti nchini hiyo, huko Addis Ababa.

Katika taarifa ya pamoja, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki wametoa wito wa kusitishwa haraka mapigano nchini Ethiopia na kuitishwa mazungumzo ya kitaifa ya pande zote kwa ajili ya kudumisha amani, utulivu, demokrasia, utawala bora na maridhiano.

Taarifa hiyo imetoa wito wa kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa raia bila ya kizuizi chochote na kulindwa haki za binadamu.

Awali Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki, alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter akikemea vikali vitendo vya kihasama vinavyoendelea nchini Ethiopia, akisisitiza kwamba njia pekee ya kutatua mzozo huo ni kusitishwa kwa mapigano mara moja na kufanya mazungumzo ya kisiasa.

Faki amesema kuwa mjumbe wa Umoja wa Afrika, rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, ataendeleza juhudi za upatanishi nchini Ethiopia.

Tigray, Ethiopia

Kwa upande wake, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Martin Griffiths, ameonya kwamba kupanuka zaidi mzozo unaoshuhudiwa nchini Ethiopia na kuwa ghasia za kikabila kunaweza kusababisha wimbi kubwa la wakimbizi linalokumbusha machafuko yaliyoshuhudiwa katika uwanja wa ndege wa Kabul wakati wa kuondolewa kwa vikosi vya kigeni nchini Afghanistan mwezi wa Agosti baada ya Taliban kushika udhibiti wa nchi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban Waethiopia milioni 26 wanahitaji msaada, ikiwa ni pamoja na watu milioni 9 wanaotegemea msaada wa chakula, wengi wao wakiwa eneo la Tigray, huku kukiwa na viwango vya juu vya utapiamlo.

Tags