Dec 04, 2021 07:32 UTC
  • UN yarefusha muda wa oparesheni dhidi ya maharamia Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa limeidhinisha kuendelea mpango ambao unaruhusu majeshi ya majini ya kimataifa kukabiliana na maharamia katika pwani ya Somalia kwa muda wa miezi mitatu mingine.

Azimio hilo ambalo limepitishwa bila kupingwa limetoa muda wa miezi mitatu kwa oparesheni hizo kuendelea huku serikali ya Somalia ikitazamiwa kutumia kipindi hicho kujitayarisha kulinda pwani ya nchi hiyo.

Hata hivyo Ufaransa imedai kuwa muda uliowekwa ni mfupi sana kwani kuondoka vikosi vya kimataifa kutaacha 'pengo la usalama' katika eneo hilo.

Mratibu wa ubalozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Sheraz Ghasri amesema uwepo wa vikosi vya kimataifa umezuia hujuma ya maharamia katika kipindi cha miaka minne.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Hata hivyo Somalia inasema baada ya kusitishwa mashambulizi ya maharamia magharibi mwa Bahari ya Hindi,  kuna haja ya vikosi vya kimataifa kuondoka katika pwani ya nchi yake. Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman amesema katika kipindi cha miezi mitatu ijayo uwepo wa vikosi vya kimataifa unapaswa kuwa katika fremu ya mapatano ya pande mbili.  Amesema kuondoka maharamia kunamaanisha kuwa uwepo wa majeshi ya kimataifa katika maji ya pwani ya Somalia ni jambo lisilohusiana na uharamia.

Somalia ilipinga vikali pendekezo la awali la Marekani la kutaka kuruhusiwa majeshi ya majini ya kimataifa yaendelee kulinda doria katika pwani yake kwa muda wa mwaka momja mwingine.