Dec 04, 2021 11:23 UTC
  • Shule zafungwa Ethiopia kwa muda wa wiki ili wanafunzi wasaidie kuvuna mazao

Wizara ya Elimu ya Ethiopia imetangaza habari ya kufungwa kwa shule zote za sekondari nchini humo ili kuwaruhusu wanafunzi kusaidia katika kuvuna chakula katika mashamba ya Waethiopia wanaopigana vita dhidi ya kundi la wapiganaji wa TPLF.

Duru za karibu na serikali ya Ethiopia zimemnukuu Berhanu Nega Waziri wa Elimu wa Ethiopia akisema kwamba shule zitafungwa kwa muda wa wiki moja ili kuwapa fursa wanafunzi hao ya kushiriki katika shughuli ya uvunaji mazao hasa katika maeneo ambayo wamiliki wake wameyaacha na kuelekea vitani kupigana bega kwa bega na jeshi la serikali dhidi ya wanamgambo wa TPLF.

Serikali ya Ethiopia ilitangaza siku ya Jumatatu kwamba zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 hawapo shule kutokana na mapigano yanayoendelea kaskazini mwa nchi hiyo. Zaidi ya shule 7,000 zimebomolewa kufuatia vita katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia na kusababisha matatizo kwa wanafunzi zaidi ya milioni moja.

 

Wakati huo, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimetoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Ethiopia, huku afisa wa UN akionya dhidi ya kukaririwa hali iliyoshudiwa Kabul nchini Afghanistan baada ya Taliban kuidhibiti nchi hiyo.

Vita hivyo nchini Ethiopia vilianza Novemba 2020 baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutoa amri ya kushambuliwa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF baada ya kuwatuhumu wapiganaji wa harakati hiyo kuwa waliwashambia askari wa jeshi la serikali kuu.

Mapigano katika jimbo la Tigray yamepelekea maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kulazimika kuishi katika mazingira magumu ya kiafya na kukabiliwa na hatari ya baa la njaa.