Dec 04, 2021 11:24 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka wafanya mapinduzi Sudan kuheshimu uhuru wa kusema

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka majerali waliofanya mapinduzi nchini Sudan kuheshimu uhuru wa wananchi wa kutoa maoni na kuacha pia kuvikandamiza vyombo vya habari.

Antonio Guterres amesisitiza kuwa, makamanda wa jeshi na waliofanya mapinduzi nchini Sudan wanapaswa kuheshimu uhuru wa kujieleza na vilevile kuhakikisha kwamba, vyombo vya habari nchini humo vinafanya shughuli zao kwa uhuru kamili pasi na kukandamizwa.

Katika ripoti yake kwa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Guterres amesema kuwa, Sudan imegeuka na kuwa anga ya chuki dhidi ya wanahabari.

Mamia ya wanaharakati wa kisiasa, waandishi habari na waandamanaji wametiwa mbaroni nchini Sudan baada ya kutokea mapinduzii ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

 

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwataka Wasudani kuwa na busara na kuafiki mapatano yaliyosainiwa kati ya Waziri Mkuu na jeshi la nchi hiyo kwa lengo la kudhamini kipindi cha amani cha mpito kuelekea kuundwa serikali ya kiraia huko Sudan.

Maandamano yamekuwa yakiendelea huko Sudan tangu Mkuu wa jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al Burhan aongoze mapinduzi tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka huu na kuvunja taasisi zote za kiutawala za serikali ya mpito sambamba na kuwafuta kazi washirika wake wasio wanajeshi ambao waligawana nao madaraka kwa mujibu wa mapatano yaliyosainiwa mwaka 2019 huko Sudan. 

Hata hatua ya jeshi ya kumrejesha tena madarakan Waziri Mkuu Abdalla Hamdok nayo haijasaidia kutuliza wimbi la maandamano nchini humo.