Dec 05, 2021 15:14 UTC
  • Rais Samia awataka Watanzania kuchukua tahadhari ya COVID-19

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka wananchi wa nchi hiyo yay Afrika Mashariki kuchukua tahadhari dhidi ya wimbi la nne la ugonjwa wa Covid- 19 huku akiwataka ambao hawajapata chanjo kwenda kuchanja akisema kuwa, ugonjwa huo hautabiri.

Mama Samia ameyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Morocco hadi Mwenge jijini Dar es Salaam yenye urefu wa Kilomita 4.3.

Rais Samia amesema kwa sababu ugonjwa huo umeanza kuoneka katika nchi za wengine na watu husafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine hakuna uhakika ni lini ugonjwa huo utaingia nchini. “Hivyo naomba kila mwananchi achukue tahadhari, hilo wimbi la nne kama litafika basi lifike likiwa na kasi ndogo ya vifo na maambukizi,” amesema Samia.

Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka watu kuiga utamaduni wa nchi ya Japan ambao wakisalimiana hawapeani mikono bali huifunga na kuinamiana.

Rais Samia Suluhu Hassan akipata chanjo ya Covid-19

 

Chini ya uongozi wa Rais Samia aliyechukua madaraka Machi 19 mwaka huu, Serikali imeweka msisitizo wa chanjo kama moja ya njia muhimu za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19. Mtangulizi wa Samia, John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 alikuwa na msimamo tofauti juu ya chanjo huku akielekeza wataalamu wake kujiridhisha, akidai baadhi ya chanjo si salama kwa Watanzania.

Hata hivyo serikali ya Tanzania tofauti na nchi nyingine za dunia imekuwa haitoi takwimu kuhusiana na maambukizo au vifo vinavyotokana na corona hatua ambayo inakosolewa na baadhi ya wajuzi wa mambo huku kukiweko na taarifa zisizo rasmi za kuweko maambukizo na vifo vya corona katika nchi hiyo.