Dec 05, 2021 15:38 UTC
  • Zaidi ya watu 100 wauawa katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi Niger

Shambulio la kigaidi dhidi ya kambi moja ya jeshi magharibi mwa Niger limepelekea zaidi ya watu 100 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Afisa mmoja wa jeshi la Niger ameziambia duru za habari kwamba, kwa akali magaidi 79 na wanajeshi 29 wa nchi hiyo wameuawa kufuatia shambulio la kigaidi dhidi ya jeshi ya Kundi la G-5 katika mji wa Tillaberi ulioko magharibi mwa nchi hiyo.

Hadi tunaingia mitamboni hakuna kundi lililokuwa limetangaza kuhusika na shambulio hilo la kigaidi ambalo limetajwa kuwa moja ya mashambulio makubwa kuwahi kutokea katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika katika siku za hivi karibuni.

Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa shambulio hilo likawa limefanywa na moja kati ya makundi yanayobeba silaha yenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya Daesh (ISIS) na al-Qaeda, ambayo yanaendesha operesheni zao katika eneo la Sahel, magharibi mwa Afrika.

Wanachama wa moja ya makundi ya wabeba silaha nchini Niger

 

Mwezi uliopita wa Novemba shambulio jingine la genge la wabeba silaha liliua watu karibu 70 wasio na hatia katika eneo la Tillaberi, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Nchi tano za eneo la Sahel ya Afrika ambazo ni Chad, Mali, Burkina Faso, Mauritania na Niger ziliuunda kundi la G-5 mwaka 2017 kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi katika mipaka ya pamoja. 

Hata hivyo vikosi vya kundi hilo vinaonekana kutopata mafanikio katika operesheni zake kwani mashambulio ya kigaidi yameongezeka na kukithiri katika miaka ya hivi karibuni katika maeneo hayo.

Tags