Dec 06, 2021 04:48 UTC
  • Adama Barrow atangazwa rasmi mshindi wa urais nchini Gambia

Maelfu ya wafuasi wa rais Adama Barrow wamemiminika mitaani kusherehekea ushindi wa rais huyo wa Gambia kwa kipindi cha pili mfululizo baada ya matokeo rasmi kutangazwa alfajiri ya leo Jumatatu. Awali Adama Barrow alisema kuwa hatogombea tena urais wa nchi hiyo, lakini hakutekeleza ahadi yake hiyo.

Barrow ambaye ushindi wake katika uchaguzi wa rais miaka mitano iliyopita ulimaliza miongo miwili ya utawala wa kidikteta wa Yahya Jammeh ameshinda kipindi cha pili cha uchaguzi wa rais kwa kupata zaidi ya silimia 53 ya kura. Mpinzani wake wa karibu Ousainou Darboe amepata asilimia 27.7 ya kura kwa mujibu wa tangazo la tume ya uchaguzi wa juzi Jumamosi. 

Mkuu wa tume ya uchaguzi ya Gambia, Alieu Mommar Njai amemtangaza Rais Barrow kuwa mshindi wa uchaguzi huo mbele ya waandishi wa habari masaa machache baada ya wagombea wa upinzani kulalamikia matokeo hayo hasa baada ya kutangazwa kwamba Barrow alikuwa anaongoza matokeo ya awali ya uchaguzi huo.

Rais Adama Barrow wa Gambia

 

Mji mkuu wa Gambia umeshuhudia wimbi kubwa la wafuasi wa Barrow wakisherehekea ushindi huo mitaani na katika barabara za Banjul, wakipiga honi na kucheza. 

Baada ya kutangazwa matokeo hayo, Rais Barrow ameahidi kufanya juhudi zake zote kuhakikisha anatumia vizuri rasilimali za Gambia kuiletea maeneo nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. 

Kabla ya kutangazwa matokeo rasmi, wagombea watatu wa upinzani walipinga matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ambayo yalionesha Barrow anaongoza.

Uchaguzi wa mara hii wa Gambia ulikuwa unafuatiliwa kwa karibu na jamii ya kimataifa kutokana na kwamba ulikuwa wa kwanza kufanyika baada ya utawala wa kidikteta wa Yahya Jammeh aliyetawala Gambia kwa muda wa miaka 22 baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagaji wa damu mwaka 1994.