Dec 06, 2021 07:13 UTC
  • Jenerali anayependa kufanya mapinduzi ya kijeshi Sudan ajipendekeza tena kwa Wazayuni

Abdul Fattah al Burhan, jenerali anayependa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan, kwa mara nyingine ameunga mkono kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya nchi hiyo na utawala dhalimu wa Kizayuni.

Jenerali al Burhan amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Arabia ya Saudi Arabia kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel eti ni nchi kama nchi nyingine duniani.

Jenerali huyo wa kijeshi ambaye hivi karibuni alifanya mapinduzi mengine ya kijeshi nchini Sudan amedai pia kuwa ni jambo la dharura kwa Sudan kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kama inataka kurejea katika kile alichodai ni jamii ya kimataifa.

Hata hivyo ameshindwa kuficha ukweli kwamba msimamo wake huo unatokana na mashinikizo ya Marekani na amedai kuwa, Washington imesema haitoiondolea vikwazo Sudan hadi pale itakapotangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Bendera ya utawala wa Kizayuni

 

Ni vyema tukakumbusha hapa kuwa, mwezi Februari 2020, Jenerali al Burhan alionana na waziri mkuu wa wakati huo wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu na tangu wakati huo hadi hivi sasa amekuwa akiisukuma Sudan upande wa kuwa na uhusiano kamili na utawala wa Kizayuni.

Baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain, Sudan ilikuwa nchi ya tatu ya Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 2020. Baada ya hapo pia, nchi nyingine ya Kiarabu yaani Morocco nayo ilifuata mkumbo huo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel kwa mashinikizo ya Marekani.