Dec 07, 2021 04:56 UTC
  • Tahadhari iliyotolewa na Algeria kuhusu njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kulidhibiti bara la Afrika

Kwa muda mrefu sasa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umetumia sera na mbinu tofauti ili kujipenyeza na kuwa na satua katika nchi za Afrika, muhimu zaidi ikiwa ni ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu; sera ambayo imeweza kutekelezwa kivitendo katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani.

Hatua hiyo imeshadidisha mvutano baina ya nchi za Kiafrika na hasa kati ya Morocco na Algeria, ambazo ni nchi muhimu katika eneo la kaskazini ya bara hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Ramtane Lamamra ametahadharisha juu ya kuongezeka, kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa, ushahwishi na satua chafu ya utawala wa Kizayuni na akasema: namna viongozi wa Morocco wananvyouhami na kuuunga mkono utawala wa Kizayuni katika eneo la Afrika Kaskazini ni dhahir shahir kwamba, satua na ubeberu wa Kizayuni umeongezeka katika eneo hili kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Ramtane Lamamra

Mbali na Imarati, Bahrain na Sudan, Morocco ni nchi ya nne ambayo mwaka uliopita wa 2020 ilikubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel; na katika muda wa miezi kadhaa sasa imepanua mahusiano yake ya kisiasa na utawala huo haramu, kiasi kwamba maafisa wa Israel wameshafanya safari mara kadhaa za kuitembelea Morocco na kutilia mkazo suala la kuimarisha uhusiano na nchi hiyo. Hivi karibuni pia, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Benny Gantz alielekea Rabat, na pande hizo mbili zikasaini makubaliano ya kuanzisha ushirikiano wa kiusalama. Baada ya kusaini hati ya makubaliano hayo, Gantz aligusia pia kustawishwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Morocco na utawala wa Kizayuni.

Kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Morocco na utawala haramu wa Kizayuni kumekoleza moto kwenye migogoro ya eneo hususan kati ya Morocco na Algeria. Israel, ambayo katika miaka ya karibuni imekuwa ikitekeleza sera ya kujipenyeza na kuwa na ushawishi ndani ya nchi za Kiafrika, hivi sasa imekamia zaidi, kuliko hata ilivyokuwa hapo kabla, kujijengea satua ndani ya nchi tofauti za bara hilo kwa visingizo vya kuzipatia misaada ya kiuchumi na kisiasa. Mashirika ya Israel yanajishusisha na mradi wa bwawa la Ethiopia la Renaissance au An-Nahdhah, ambalo limekuwa chanzo cha mvutano na mgogoro kati ya nchi hiyo na majirani zake Misri na Sudan. Aidha kwa kutumia mashauriano ya kighilba, na licha ya upinzani wa nchi 14 wanachama wa Umoja wa Afrika, zikiwemo kadhaa za Kiarabu, Israel imefanikiwa kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo. Kwa hatua yake ya kustawisha uhusiano na Morocco, utawala haramu wa Kizayuni umesababisha mivutano ndani ya bara la Afrika.

Bwawa la Ethiopia la Renaissance au An-Nahdhah

Ukweli ni kwamba, mbali na kupanua satua yake ili kuweza kunufaika na suhula na maliasili za nchi za Afrika, utawala wa Kizayuni umedhamiria kusaini pia mikataba mbalimbali ya kijeshi na kiusalama ili kujipanua na kujiimarisha katika kukabiliana na washindani wake katika nchi za bara hilo. Aidha Israel inapigania kustawisha uhusiano na nchi za Kiarabu za bara Afrika ili kuvutia uungaji mkono wa nchi hizo katika kufanikisha sera zake za kichokozi na kivamizi dhidi ya Wapalestina.

Ahmad Ibrahimi, mratibu wa vuguvugu la wananchi nchini Algeria linalopinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni amesema: kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni ni jinai na uhalifu dhidi ya haki za taifa la Palestina na ni tishio kwa amani na usalama wa Waarabu na Waislamu. 

Israel inatekeleza sera hiyo wakati nchi hizo siku zote zimekuwa zikipinga siasa na sera za kivamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu za utawala huo wa kizayuni, sambamba na kutetea haki za Wapalestina; na hata hivi sasa pia licha ya baadhi ya tawala za Kiarabu ukiwemo wa Morocco kukubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, raia wa nchi hizo wanaendelea kupinga hatua hiyo. Ni kama ilivyoshuhudiwa wakati waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni alipotembelea Morocco, ambapo maelfu ya watu walimiminika mabarabarani na kuandamana huku wakitoa kaulimbiu za kutaka kufutwa mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kuvunjwa ushrikiano wa kijeshi na kiusalama ulioanzishwa kati ya nchi yao na utawala huo haramu.

Muhammad al Ghafri, mratibu wa mtandao wa kidemokrasia wa kutangaza mshikamano na wananchi wa mataifa aliyeko nchini Morocco amesema: kinyume na zilivyofanya tawala za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, wananchi wa mataifa ya Kiarabu wanapinga kuanzishwa uhusiano huo na wanajitokeza mitaani na mabarabarani kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina. 

Hata kama viongozi wa utawala haramu wa Kizayuni wakiungwa mkono na Marekani, wangali wanafanya juu chini ili kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu, lakini inavyoonyesha, nchi hizo, ambazo zina tajiriba ya kutawaliwa na wakoloni si tu haziko tayari tena kukubali siasa na sera hizo, lakini pia zitaendeleza jitihada za kutetea malengo matukufu ya Palestina kwa kuimarisha umoja na mshikamano baina yao. Kuhusiana na nukta hiyo Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesema: kuna irada na matashi ya nje yanayojaribu kuusogeza utawala wa Kizayuni karibu na mipaka yetu, lakini inapasa tutatue matatizo yetu sisi wenyewe; na kwa udugu na mshikamano tufanye juhudi ili tuweze kupata njia bora ya kujikwamua kwenye migogoro ya pande kadhaa na njama zilizoilenga nchi yetu.../

Tags