Dec 07, 2021 15:57 UTC
  • Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania aomba Wimbo wa Taifa ubadilishwe

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Fredrick Shoo, ameomba neno HAKI liongezwe katika wimbo wa taifa hilo, akisisitiza kuwa ni tunda la amani ya nchi.

Askofu Shoo ametoa wito huo wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu iliyofanyika mkoani Kilimanjaro.

Huku akiuimba wimbo huo, Askofu Shoo ameshauri katika mstari unaopatikana kwenye ubeti wa kwanza wa 'Mungu ibariki Tanzania, dumisha uhuru na umoja', liongezwe neno haki.

"Haki ni jambo la msingi, wanasema pasipo haki hakuna amani. Amani ni tunda la haki, sijui, lakini nina ndoto na hivi nimeanza sijui, kama navunja sheria, tunavyoimba wito wa taifa mimi siku hizi kimya kimya nasema dumisha uhuru, haki na umoja, " amesema Askofu Shoo.

Kiongozi huyo wa dini ameshauri mstari huo uimbwe 'Mungu ibariki Tanzania, dumisha uhuru, haki na umoja', kwani ni dua inayopelekwa kwa Mungu.

Ameongezea kwa kusema, anaamini utafika wakati itakubalika hivyo.

Aidha, Askofu Shoo amewaomba viongozi wa dini wawe mstari wa mbele katika kushiriki kwenye masuala ya kidemokrasia, kisiasa na kijamii kwani ushiriki wao unaleta tija kwenye uongozi na utawala ndani ya jamii.

Vilevile, Mkuu huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania amesema, viongozi wa dini wanapaswa kuwa na maarifa na uweledi ili kuzilinda na kuzitetea haki za msingi za watu na jamii wanayoishi na kuwaongoza kama viongozi wao wa kiroho, kwani bila kufanya hivyo haki za msingi za watu zitakuwa zinavunjwa kwa kuwa hakuna wa kuwatetea na kuwasemea.../

 

 

 

Tags