Dec 24, 2021 02:50 UTC
  • Wabunge Senegal wawasilisha muswada dhidi ya ushoga

Kundi la wabunge nchini Senegal limewasilisha muswada bungeni ili kutilia mkazo na kulipa nguvu suala la kutokomeza vitendo vya ushoga na mahusiano ya watu wenye jinsia moja katika nchi hiyo ya Maghariibi mwa Afrika yenye raia wengi Waislamu.

Muswada huo umewasilishwa na kundi la wabunge wa upinzani katika Bunge la Senegal. Itafahamika kuwa si kinyume cha sheria kujiarifisha kama mtu mwenye mahusiano ya jinsia moja au shoga katika nchi hiyo inayohesabiwa kuwa ni taifa la  kihafidhina na la Kiislamu lakini kitendo chochote cha ushoga au kuwa na mahusiano ya jinsia moja nchini humo adhabu yake ni kifungo cha jela hadi miaka mitano.  

Mamadou Lamine Diallo mbunge wa upinzani katika Bunge la Senegal amesema kuwa wananchi wote wa nchi hiyo wanaunga mkono muswada  huo. Amesema, ni vyema kwa Marekani, Canada, Ufaransa na Ulaya kufahamu kuwa suala hilo linawahusu wananchi wa Senegal wenyewe. 

Wananchi wa Senegal wanataraji kuwa, muswada huo dhidi ya ushoga na mahusiano ya jinsia moja utapasishwa na bunge la taifa la nchi hiyo kwa uungaji mkono wa viongozi wa dini, viongozi wa vyama na vijana, kwa sababu hilo ni takwa la jamii nzima. 

Muswada huo umekusudia kufanyiwa marekebisho sheria ili hukumu  ya kuanzia miaka mitano hadi kumi jela iweze kutolewa pamoja na faini ya dola kuanzia 1800 hadi dola 8000 kwa mtu yoyote atakayepatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo hivyo vilivyo kinyume na maumbile ya mwanadamu. Watu watakaopatikana na hatia hiyo hawatakuwa na haki ya kukata rufaa.  

Wasenegali wakiandamana kupinga ushoga

Tarehe 23 mwezi Mei mwaka huu mamia ya wananchi wa Senegal waliandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Dakar, wakiitaka serikali kupasisha sheria ya kupiga marufuku ushoga nchini humo haraka iwezekanavyo.

Tags