Jan 01, 2022 12:38 UTC
  • Rais Museveni asema shule zitafunguliwa Uganda mwezi huu

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kuwa, shule za nchi hiyo ambazo zilikuwa zimefungwa tokea Machi 2020 kutokana na msambao wa maradhi ya Covid-19, sasa zitafunguliwa mwezi huu wa Januari, 2022.

Rais Museveni alitangaza hayo jana usiku katika ujumbe wake wa mwaka mpya wa Miladia na kuongeza kuwa, sasa shule na sekta nyingine za uchumi zilizokuwa zimefungwa kwa miezi kadhaa nchini humo ili kutekeleza sheria na masharti ya kukabiliana na wimbi la maambukizo ya kirusi cha corona, zitafunguliwa Januari mwaka huu wa 2022.

Amesema shule za chekechea, za msingi na sekondari zitafunguliwa Januari 10. Ameongeza kuwa, shughuli katika mabaa na kumbi za starehe zitarejea tena, sambamba na kuondolewa agizo la kutotoka nje usiku, wiki mbili baada ya shule kufunguliwa.

Msambao wa Corona umepelekea kufungwa aghalabu ya shule duniani

Kwa mara ya kwanza Uganda ilifunga shule mnamo Machi mwaka juzi (2020), muda mfupi baada ya mripuko wa kwanza wa virusi vya corona kuthibitishwa kwenye bara la Afrika.

Rais wa Uganda amewaasa wananchi wa nchi hiyo kupiga chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, akisisitiza kuwa hilo ndilo suluhisho kuu la kupambana na janga la corona.

Kufikia jana Ijumaa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilikuwa imenakili kesi zaidi ya 137,000 za maradhi hayo hatari ya kuambukiza, mbali na vifo 3,300.

Tags